Samia: Mwelekeo safi mashirika ya umma

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mashirika ya umma yana mwelekeo mzuri na yanajenga heshima ya nchi kutokana na mageuzi wanayofanya na gawio wanazotoa.
Amesema wakisimamia vema utendaji wa taasisi hizo wananchi wataona faida za uwekezaji na wataongeza mchango wao kwenye Pato la Taifa sambamba na kupunguza deni la taifa.
Akizungumza katika Siku ya Gawio 2025 Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Samia amesema gawio wanalopokea ni kielelezo cha juhudi, uaminifu na uadilifu katika kusimamia rasilimali za umma hivyo wanapaswa kuwa mfano wa ufanisi, uwajibikaji na tija.
Alisema gawio si fadhila bali ni haki ya umma kupitia uwekezaji mkubwa uliofanywa katika mashirika hayo ambayo thamani yake imefikia Sh trilioni 86.29.
Rais Samia alisema kwa jinsi wanavyopandisha gawio ndivyo ulimwengu utakavyowaheshimu na kwamba itawezesha kupunguza mzigo wa deni la taifa.
Alisema mwaka jana kipindi kama hiki alipokea Sh bilioni 611 kama gawio na michango kutoka katika taasisi na mashirika ya umma. Alisema hadi kufikia Juni 30, 2024 jumla ya kiasi kilichokusanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ni Sh bilioni 767.
“Leo Juni 10, 2025 nimekabidhiwa Shilingi trilioni 1.028, ni ongezeko la asilimia 68 ya kiasi nilichokabidhiwa mwaka jana kipindi kama hiki, na ongezeko la asilimia 34 zaidi ya makusanyo yote ya mwaka 2023/2024 na makusanyo bado yanaendelea. Hakika mavuno nimeyaona na kuyashuhudia,’’ alieleza Rais Samia.
Alisema lengo lao ni kufikia angalau Sh trilioni 1.5 kwa mwaka ujao na kwamba wana imani watafikia. Alisisitiza: “Leo hii tumepokea trilioni moja, ni pesa kubwa na itakwenda kutufaa kwenye mambo kadhaa.
Imepunguza utegemezi tuliokuwanao huko nyuma, kama tulikuwa tunagaiwa trilioni kumi sasa moja tumeileta wenyewe ndani mtategemea tisa, tukienda hivyo kila mwaka tutapunguza utegemezi na kujitegemea na ndivyo mashirika yetu yanatakiwa kufanya kazi,” alibainisha Rais Samia.
Alisema mageuzi waliyoyafanya yamechangia mashirika 11 ya kipaumbele kati ya 13 yaliyokuwa na mtaji hasi kutoka kwenye kundi hilo na kuingia kwenye orodha ya mashirika yenye mitaji chanya.
“Mashirika mengine manane kati ya 13 yaliyokuwa yakipata hasara mfululizo yametoka kwenye lindi hilo na sasa yanapata faida. Naamini mashirika haya yanaweza kufanya vizuri zaidi,” alieleza.
Aliongeza: “Nimejulishwa katika kipindi hiki Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Shirika la Maendeleo la Petrol (TPDC) zimejitoa kuitegemea serikali na badala yake wanajitegemea wenyewe kwa mishahara na uendeshaji na kwamba kwenye miradi ya maendeleo ndio watakapoifuata serikali”.
Alieleza kukamilika kwa dashibodi ya watumishi wa umma itachangia usimamizi mzuri wa mashirika na itatoa
fursa ya kuona yanayofanya vizuri na yanayoshuka.
Pia, itapunguza muda wa ufuatiliaji, kurahisisha kufanyika maamuzi ya kiutendaji na kimkakati katika ngazi zote. Alisema mageuzi hayo yatahusisha kutungwa kwa sheria na ikikamilika itaimarisha usimamizi wa rasilimali zilizowekezwa kwenye mashirika.
Alisema mashirika ya umma yanapaswa kuwajibika na kuleta tija iliyokusudiwa kwa maendeleo ya nchi kwa kuchangia angalau asilimia 10 ya mapato yote.
Ametoa maagizo manne ikiwamo taasisi za umma kuwa wabunifu kuongeza ufanisi katika utendaji na kutatua changamoto zinazowakabili ikiwamo ya mitaji.
Rais Samia ambaye alimsifu Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu kwa kazi nzuri ya, kusimamia mashirika hayo, alielekeza watumie fursa mbalimbali zinazowazunguka katika kutatua changamoto hizo ikiwamo soko la hisa.
“Msajili wa Hazina nakuagiza ukafanye utafiti ili kuja na mapendekezo ya taasisi zinazopendekezwa kujiorodhesha katika soko la hisa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu, lengo ni kuwapa wananchi nafasi ya kumiliki mashirika haya na hatimaye kufikia maelekezo yangu ya mashirika ya umma kumilikiwa na wananchi badala ya kuwa mashirika ya serikali,” alieleza Rais Samia.
Amemtaka Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kusimamia ukamilishaji wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma ili kuwa na Mfuko wa Uwekezaji na kuwezesha usimamizi madhubuti wa uwekezaji wa serikali unafikiwa.