Samia na hotuba ya matumaini uzinduzi wa kampeni CCM
AGOSTI 28, 2025 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilianza safari ya kuwania kushika dola kwa mara nyingine kupitia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Uzinduzi wa safari hiyo ulifanyika Kawe, Dar es Salaam na CCM kutambulisha wagombea wake ambao ni Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza wake, Dk John Nchimbi.
Akizungumza na wanaCCM na wananchi waliofurika katika uzinduzi huo, Samia anasema, “Uchaguzi huu si wa kuchangua viongozi tu, bali ni kuchagua kuendeleza safari yetu ya kuinua na kuendeleza hali ya maisha ya Watanzania wote na kuimarisha ustawi wa jamii.”
Anasema, “Pia ni fursa ya kuchagua kuendeleza maono ya kujenga Tanzania imara, yenye ustawi na inayojitegemea. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakuja kwenu kuomba tena ridhaa na dhamana ya kuiongoza Serikali na Taifa la Tanzania.”
Rais Samia anaongeza katika uzinduzi huo wa kampeni za CCM: “Tunakuja tena tukiwa na sababu kuu mbili. Kwanza, tumefanya vema na tumefanikiwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020-2025 na pili ni CCM tunaamini katika kulitumikia Taifa.”
SOMA: CCM yafunika Dar, Samia aahidi makubwa siku 100 ofisini
Kwa upande wake, Mgombea Mwenza wa CCM, (Dk Nchimbi) yeye anasema, “Niko tayari, niko timamu kutekeleza maelekezo yako (Mwenyekiti wa CCM Rais Samia) na ya chama chetu kutafuta ushindi wa chama chetu na baadaye kufanya kazi kwa juhudi kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.”
Akibainisha ahadi ya mambo atakayotekeleza ndani ya siku 100 anasema ni pamoja na kuendelea na mabadiliko yanayogusa moja kwa moja maslahi na ustawi wa maisha ya wananchi. “Tumefungua ukurasa mpya wa matumaini kwa taifa letu, safari ya kutekeleza Dira ya Maendeleo 2050 imeanza,” anasema.
Anataja mambo hayo muhimu kuwa ni pamoja na kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Kuhusu suala hili Rais Samia anasema Serikali atakayounda itazindua rasmi Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote kwa awamu ya majaribio kwa kuanza na wazee wajawazito, watoto na watu wenye ulemavu.
Anasema, “Gharama za matibabu kwa makundi haya zitabebwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.” Kwa mujibu wa mgombea urais huyo wa CCM ambaye ni Rais wa Tanzania, pia serikali itaanza kugharamia kwa asilimia 100 matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wasio na uwezo kwa magonjwa yasiyo ya kuambukizwa.
Magonjwa hayo ni pamoja na saratani, figo, moyo, sukari, mifupa na mishipa ya fahamu. “Haya ndio magonjwa yenye gharama kubwa ambayo wananchi wasio na uwezo wamekuwa wakishindwa kumudu gharama zake,” anabainisha.
Anasema ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya, Serikali itaajiri wahudumu wa afya wapya 5,000 ndani ya siku 100 wakiwemo wauguzi na wakunga ili kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Kwa mujibu wa Samia, eneo lingine ni serikali kupiga marufuku hospitali zote nchini na kuzitaka kuacha kuzuia miili ya marehemu kuchukuliwa na ndugu zao hata kama gharama za matibabu aliyopatiwa marehemu hazijalipwa.
“Tutakuja na mfumo mwingine utakaohakikisha jamaa wa marehemu wanalipa gharama, lakini si kuzuia miili ya watu waliotangulia mbele za haki,” anasema.
Kuhusu sekta ya elimu, anasema serikali yake itaandaa mkakati madhubuti wa kisayansi kuhakikisha kila mtoto wa darasa la tatu anaweza kusoma, kuhesabu na kuandika bila shida. “Kulitimiza hili, tutaajiri walimu 7,000 wa masomo ya Hisabati na Sayansi,” anabainisha.
Hatua nyingine Samia anasema Serikali yake itazindua mpango wa pamoja kati ya waajiri, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vikuu kuwianisha mafunzo na mahitaji ya sekta za kipaumbele kama nishati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), viwanda vya kuongeza thamani na kuwafanya wanafunzi wa Veta waweze kuchukuliwa viwandani ili kufanya mazoezi.
Mgombea huyo wa CCM anasema Serikali ijayo itatenga Sh bilioni 200 kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati na kuwezesha uendeshaji wa kampuni changa.
“Tutarasimisha sekta isiyo rasmi ikiwamo sekta ya akina mama lishe, maofisa usafirishaji maarufu kama bodaboda na bajaji na wajasiriamali wadogo watarasimishwa ili waingie katika mfumo rasmi wa serikali na waweze kupata huduma zao na wenyewe waweze kushirikiana na serikali,” anasema.
Rais Samia anasema pia Serikali yake itaanzisha programu maalumu ya ujenzi wa mitaa ya viwanda wilayani ili kujenga na kuzalisha ajira kwa Watanzania kupitia kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, madini na msitu pamoja na uzalishaji wa vifaa vya ujenzi.
Anasema pia serikali itaanza utekelezaji wa ujenzi wa gridi ya taifa ya maji ili kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji kwa matumizi ya nyumbani, kilimo, mifugo na biashara. “Gridi ya taifa ya maji itahusisha vyanzo vikubwa vya maji kutoka Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa pamoja na mito mikubwa nchini,” anasema.
Anaongeza kuwa, Serikali yake itaendeleza jitihada za matumizi ya nishati safi ya kupikia hatua itakayopunguza utegemezi wa kuni na mkaa na kuweza kuhifadhi mazingira. Anasema pia itaanzisha mifumo rafiki ya uwajibikaji ambapo mawaziri, wakuu wa mikoa na watendaji wengine wa Serikali watatoa taarifa na kujibu maswali kutoka kwa wananchi kwa njia ya kidijiti na ujumbe mfupi wa bure.
Rais Samia anasema: “Kutakuwa na mifumo hiyo na hiki ndicho kitakuwa kipimo cha mawaziri, ameulizwa shida ngapi, amejibu ngapi amechukulia hatua ngapi, hiki ndicho kipimo chao.”
Anasema: “Huku serikali yake ikiongozwa na Falsafa ya R4, tutaendeleza mashauriano na wadau wa siasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi kwa kuunda tume na kuanzisha mazungumzo ya maridhiano na upatanishi pamoja na kuandaa mazingira ya kuanza mchakato wa katiba mpya.”
“Kwa ujumla, katika miaka mitano ijayo tumejipanga kuongeza nguvu si tu kwenye miundombinu, bali pia katika ubora wa huduma zinazotolewa, kusimamia haki, amani na utulivu wa kisiasa ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo na ustawi wa taifa letu,” anasema na kuomba wananchi kwenda pamoja katika safari ya maendeleo inayomhusu kila Mtanzania.
Anatoa mwito kwa wakulima na wafanyakazi kuwa mstari wa mbele kujenga taifa linalojitegemea pamoja na vijana ambao ndio nguvukazi yenye ari na ubunifu wanaojenga kesho bora ya taifa. Katika uzinduzi huo, mgombea urais huyo wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 anasema, “Kwa wanawake na makundi mbalimbali wenye matumini ya kujenga taifa lenye ustawi na maendeleo jumuishi wote.”
Anaongeza: “Twende tujenge taifa letu, twendeni pamoja, tukachague Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili haya niliyoyaeleza yaweze kufanyiwa kazi.” Mwenyekiti huyo wa kitaifa wa CCM Taifa, anaongeza kuwa: “Leo (Agosti 28, 2025) tunaanza rasmi kampeni mimi na mgombea mwenza tutazunguka kila pahala ndani ya nchi yetu
kuwaeleza wananchi yale tunayokusudia kuyafanya.”
“Niwatake wagombea na viongozi wote wanaogombea, twendeni kwa wananchi, mtaa kwa mtaa kijiji kwa kijiji, nyumba kwa nyumba tukaeleze kazi iliyofanywa na Chama Cha Mapinduzi na yale ambayo CCM imepanga kuyafanya miaka mitano ijayo ili wananchi watupe ridhaa ya kwenda kuyatekeleza,” anaeleza.
“Wananchi niwaombe tujitokeze kwa wingi kusikiliza sera na mipango ya Chama Cha Mapinduzi ili mfanye uamuzi sahihi ya kuchagua wagombea kwa nafasi ya urais wabunge na madiwani,” anasema na kuongeza: “Safari yetu inaendelea na nguvu yetu iko katika umoja wetu, amani yetu na mshikamano wetu chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).”
Aidha, anasema anataka kuona utayari wa wanaCCM na wananchi kwa kukichangua Chama Cha Mapinduzi wa maisha ya wananchi moja kwa moja. Aidha, Rais Samia anatumia fursa hiyo kubainisha baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake cha uongozi ambapo kupitia Falsafa ya 4R Tanzania inaongoza kwa amani
na utulivu kwa mujibu wa ripoti za kimataifa Afrika Mashariki.
Anasema wakati anaingia madarakani, alikuta changamoto ya uhuru wa vyombo vya habari na kuweka wazi utashi wa kisiasa na misingi ya kisheria kwa kuondoa kifungoni magazeti yaliyofungiwa, kuboresha sheria ya habari, kutoa leseni zaidi ya 1,000 kwa magazeti, redio zaidi ya 200, mtandao ya kijamii zaidi ya 300 na blogu zaidi ya 70.
Katika kudhibiti rushwa na ufisadi, Serikali imeimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Anasema hatua hiyo imewezesha Tanzania kushika nafasi ya 82 kutoka nafasi ya 87 kati ya nchi 170 zilizofanyiwa tathmini duniani.
ITAENDELEA…



