RAIS Samia Suluhu Hassan amewatakia Waislamu wote mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa twitter, Rais Samia ameandika: “Katika mwezi huu wa ibada na toba tuendelee kuiombea nchi yetu amani, upendo, mshikamano, utulivu na haki; nguzo zenye kuleta ustawi zaidi kwa maendeleo ya nchi yetu, Ramadhan Kareem.”
Pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewatakia Waislamu mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kupitia ukurasa wake kwenye twitter Majaliwa aliandika: “Ninaungana na Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwatakia Waislamu wote mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.” Waislamu nchini walianza kufunga jana.
Juzi Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir bin Ally aliwaomba wafanyabiashara wasipandishe bei za bidhaa.
Shehe Mkuu Zubeir alisema hayo Dar es Salaam wakati akikabidhi msaada wa futari kwa familia 550 zenye hali duni kiuchumi mkoani humo.
Alisema ni vibaya kwa wafanyabiashara kupandisha bei kiholela kwa lengo la kupata faida kubwa lakini ni vibaya zaidi kupandisha bei wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa sababu watawaumiza Waislamu wanaoteseka kwa kushinda njaa kwa ajili ya kumtukuza mola wao.
Shehe Mkuu Zubeir alisema mfungo wa Ramadhani ni chuo kwa Waislamu kwa sababu unafundisha mambo yanayomjenga katika maadili na tabia njema.
“Waislamu ndani ya Mwezi wa Ramadhani wanajifunza subira, ustahimilivu na upendo, kuwa wakarimu na kuwakaribisha wenzake, hufundisha kuwa mtoaji sana na kukaribisha watu katika futari,” alisema.
Mkurugenzi wa Idara ya Da-awa na Tabligi Bakwata makao makuu, Arif Yusufu Abdulrahman alisema futari hiyo kwa familia 550 imejumlisha kila moja kupata kilo 20 za mchele, mafuta ya kula lita tano, unga wa sembe kilo tano, maharage kilo tano na sukari kilo tatu.
Yusufu alisema kilichofanyika katika ofisi za Bakwata makao makuu kitaendelea katika mikoa mbalimbali katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.