Samia: Tunzeni siri

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka watunza kumbukumbu na nyaraka (TRAMPA) na makatibu mahsusi (TAPSEA) kuzingatia kiapo cha uaminifu katika kutunza siri kwa kuwa kina maana kubwa katika utendaji wa kazi zao. Pia aliwataka watunza kumbukumbu na nyaraka na makatibu mahsusi hao kuzingatia nidhamu na uadilifu kwa kuwa mambo hayo mawili yanazaa ufanisi.

Alibainisha hayo wakati akifunga mafunzo ya uadilifu na utunzaji siri kwa watunza kumbukumbu na nyaraka na makatibu mahsusi kwenye mkutano uliofanyika Fumba, Zanzibar jana. Kutokana na umuhimu wa kiapo hicho cha uaminifu cha kutunza siri walichokula mbele ya Wakili Mkuu wa Serikali na yeye kushuhudia, aliwataka wakizingatie kwa kuwa kina maana katika utendaji kazi wao wa kila siku.

“Sasa kati yenu mtu akienda kinyume na kiapo chake alichokula akishuhudiwa na Rais wa nchi, tutajuana huko mbele kwa mbele, kwa hiyo naomba muishi kiapo chenu,” alisisitiza Rais Samia.

Aidha, kwa kuwa kaulimbiu ya mkutano huo wa kitaaluma wa Trampa na Tapsea ilisema: ‘Nidhamu, uadilifu na utunzaji siri sehemu za kazi ni chachu ya maendeleo kitaaluma’, aliwataka wajue kuwa ufanisi maana yake ni kuikamilisha kazi inavyotakiwa, kwa kiwango kinachotakiwa na kwa wakati unaotakiwa.

Alisema mtu akiwa na nidhamu na uadilifu, atazalisha kazi kwa wakati, kwa kiwango kinachotakiwa na muda unaotakiwa, hivyo alikubaliana na kaulimbiu hiyo ambayo siyo tu kwamba ni chachu ya maendeleo

kitaaluma bali kwa maendeleo ya nchi pia. Katika hatua nyingine, Rais Samia alisema ni muhimu kwa waajiri na wakuu wa taasisi katika sekta ya umma na sekta binafsi kuwaruhusu watunza kumbukumbu na nyaraka na makatibu mahsusi kushiriki mafunzo ya uadilifu na utunzaji siri ili kuwajengea uwezo na ufanisi katika kazi zao.

Katika hilo, aliwaagiza Mawaziri wa Utumishi, Ajira na Kazi kuzungumza na waajiri hususani wa sekta binafsi ili wawaruhusu wafanyakazi wa kada hizo kushiriki mafunzo hayo.

Kwa kuwa Rais Samia kitaaluma pia ni mtunza kumbukumbu na nyaraka, alisema kundi hilo pamoja na makatibu mahsusi walikuwa wameachwa nyuma kwa muda mrefu, hivyo ameamua kuwainua kutokana na unyeti wa kazi wanazofanya.

“Anayekujua ndiye anayekuthamini, asiyekujua hawezi kukuthamini, inawezekana wenzangu walivyotoka shule moja kwa moja wakaenda nafasi za juu, mimi nilianza kama muweka kumbukumbu, ni taasisi ninayoijua vizuri na ndiyo maana ninawathamini, nikiwa muweka kumbukumbu nilifanya kazi kwa karibu zaidi na makatibu muhsusi,” alisema Rais Samia.

Kuhusu ombi la Trampa kutaka kituo chao watakachojenga Dodoma kupewa jina la Rais Samia, alisema hawezi kukubali ombi hilo kwa sasa mpaka hapo kituo hicho kitapokamilika na wataona wakipe jina gani.

Katika hatua nyingine, alivitaka vyama hivyo vya Trampa na Tapsea kuiga mfano wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuanzisha mifuko yao kisheria itakayowasaidia kutatua shida zao mbalimbali. Kutokana na umuhimu wa mkutano huo wa pamoja wa Tapsea na Trampa, Rais Samia alisema mwaka 2025 utafanyika Pemba na mwakani utafanyika mkoani Mwanza.

Katika tukio hilo la jana, Rais Samia alimkabidhi hati ya kiwanja Mwenyekiti wa Trampa, Devotha Mrope kwa ajili ya kujenga kituo chao jijini Dodoma huku Trampa na Tapsea wakimkabidhi Rais Samia tuzo ya pongezi na shukrani kwa kutambua kazi anazofanya kwa Taifa.

Habari Zifananazo

Back to top button