Samia: Watumishi wa umma tekelezeni majukumu kwa weledi

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo, wakizingatia viapo vyao kwa vitendo.
Rais Samia ameyasema hayo leo alipokuwa akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ambayo pia ilihusisha kiapo cha maadili kwa viongozi waliokwishateuliwa siku za nyuma.
Viongozi walioapishwa ni Prof. Tumaini Joseph Nagu aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya afya; Dk Blandina Buganzi Kilama aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia biashara na ubunifu; na Jaji Mstaafu John Samweli Mgetta aliyeteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Maadili.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu Rais Samia amewataka viongozi hao kushirikiana kikamilifu katika kazi na watumishi wa ofisi wanazokwenda, kuheshimu maadili ya utumishi wa umma na kuwa mfano wa uongozi bora kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Kadhalika, Rais Samia amewaagiza viongozi wa Tume ya Mipango kushirikiana katika uratibu wa miradi mikubwa ya kitaifa na kuhakikisha kuwa inafungamana na malengo ya kitaifa;
Kwa upande wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Rais Samia amelielekeza Shirika hilo kuendeleza vyanzo vidogovidogo vya uzalishaji umeme nchini, kusimamia usambazaji wa umeme wa uhakika unaozalishwa pamoja na kutathmini uzalishaji umeme kwa vyanzo vya nishati jadidifu.