Sanga akagua miradi Kigamboni

DAR ES SALAAM: Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Haran Sanga, amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika jimbo hilo, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miundombinu inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi.

Katika ziara hiyo iliyofanyika Februari 24, 2026 jijini Dar es Salaam, Sanga alitembelea mradi wa ujenzi wa Daraja la Nguva pamoja na vipande vyake, lenye urefu wa mita 60, ambalo limegharimu Sh bilioni 9.2.

Aidha, alikagua mradi wa ujenzi wa Daraja la Kisarawe II lenye urefu wa mita 15, lenye thamani ya Sh bilioni 9.4, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 82.

Mbali na madaraja hayo, mbunge huyo pia alikagua ujenzi wa barabara ya Kibada–Mwasonga–Tundwisongani–Kimbiji yenye urefu wa kilomita 41. Mradi huo unaogharimu Sh bilioni 83 bila VAT, unahusisha pia ujenzi wa madaraja mbalimbali ndani ya barabara hiyo, ikiwa ni jitihada za kuboresha mawasiliano na usafirishaji katika maeneo hayo.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Sanga aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kutoa kipaumbele kwa ajira kwa wazawa wa Kigamboni ili wananchi wanufaike moja kwa moja na miradi inayotekelezwa katika eneo lao. Pia aliwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa kipindi cha miaka 20 hadi 30 kama ilivyokusudiwa.

Hata hivyo, Mbunge huyo alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele Kigamboni katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisema hatua hiyo imekuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa jimbo hilo.

Kwa upande wao, wananchi wa Kigamboni wameishukuru Serikali kupitia mbunge wao kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, wakieleza kuwa barabara na madaraja hayo yatamaliza changamoto ya usafiri iliyokuwa ikiathiri shughuli zao hasa katika kipindi cha mvua.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button