SBL yakabidhi mradi wa maji wa Sh mil 293

SBL yakabidhi mradi wa maji wa Sh mil 293

KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL) imekabidhi mradi wa maji wa Kihanju uliopo Itigi mkoani Singida ambao umefadhiliwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na WaterAid.

Mradi huo wenye uwezo wa kuhudumia watu 2,000 moja kwa moja umegharimu zaidi ya Sh milioni 293.

Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti akikabidhi mradi huo alisema kampuni imeendelea kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama kwa jamii zenye uhitaji wa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kusaidia jamii.

Advertisement

“Mradi wa Kihanju ni moja kati ya miradi kadhaa ambayo tumekuwa tukiifadhili ikiwa ni mchango wa SBL katika kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama. Kupitia programu yetu ya ‘Maji ni Uhai’ tumeweza kusaidia maeneo mbalimbali hapa nchini kuweza kunufaika na huduma hii,” alisema.

Ocitti alisema kuanzia mwaka 2010 imekuwa ikifadhili miradi ya maji na imetumia Sh bilioni 1.1 kwa ajili ya kuchimba visima 19 katika sehemu mbalimbali ambavyo vimeweza kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo.

Alisema Kampuni hiyo tayari imeshasaidia uchimbaji wa visima vya maji katika mikoa ya Iringa, Singida Kilimanjaro, Mwanza, Tanga, Ruvuma, Dar es Salaam, Pwani, Dodoma na Mara ambavyo vimesaidia upatikanaji wa maji kwa watu zaidi ya milioni mbili kwa maeneo hayo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba aliishukuru kampuni ya SBL kwa kutoa msaada huo uliokuwa ukihitajika na kuongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo hapa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkaazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga alisema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na SBL katika kutekeleza miradi ya maji ambayo imeboresha maisha ya Watanzania wengi waishio sehemu yenye changamoto ya maji safi na salama.