SBT, PBZ kuipa Zanzibar mikopo miradi ya maendeleo

ZANZIBAR: Benki ya Stanbic Tanzania (SBT) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) zimeungana kwa pamoja kuiwezesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupata mikopo ya kibenki, ili kusaidia kufadhili miradi ya maendeleo endelevu visiwani humo.
Kupitia makubaliano haya, benki hizi zitatoa jumla ya Sh bilioni 185 katika awamu ya kwanza ya mkopo huu kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mkataba huo wa ushirikiano ulisainiwa siku ya jana katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya, ambaye alisema ufadhili huo utasaidia kuimarisha uchumi wa Visiwa vya Zanzibar na kuchochea maendeleo yake kwa ujumla.
Kwa kuongezea waziri huyo alisema kuwa utiaji wa saini wa mkopo huo umekuja wakati muafaka, kwani utasaidia kuharakisha ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 7.3 ya sasa hadi zaidi ya asilimia 7.4.
“Lakini pia utatoa fedha zinazohitajika kwa ajili ya uwekezaji katika miundombinu ya kiuchumi, kuboresha sekta muhimu kama utalii, ambayo iliathirika sana na misukosuko ya janga la COVID-19,” alisema Dkt Mkuya.
Aidha, alieleza kuwa uchumi wa Zanzibar ulishuka hadi asilimia 1.2 mwaka 2022 kutokana na athari za COVID-19, lakini sasa unazidi kuimarika na utaendelea kuboreka zaidi endapo mikopo ya aina ya Stanbic na PBZ itapatikana.

Kwa mujibu wa waziri Mkuya, kutokana na kuzidi kuimarika na kuboreka kwa uchumi huo, sasa hivi kuna ongezeko la hamasa kutoka kwa benki za biashara za Tanzania Bara kuwekeza Zanzibar, ikiwemo benki ya Stanbic, ambayo inatarajia kufungua tawi lake la kwanza visiwani humo mwaka huu.
Akizungumza hapo awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ya Zanzibar, Dk Juma Malik Akil, alisema kuwa mkopo huo wa pamoja ni sehemu muhimu ya mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kukopa ndani ya nchi ili kukidhi shilingi trilioni 1.7 katika bajeti ya maendeleo ya mwaka huu wa fedha.
“Bado tunakabiliwa na pengo kubwa la ufadhili wa miradi ya maendeleo, ambalo linahitaji msaada wa aina hii na ushirikiano wa kimkakati, kama huu wa leo kati ya Benki ya Stanbic na PBZ Bank,” alisema Dk Akil.
Katika hotuba zao, viongozi wa benki hizo mbili walisema kuwa mkopo huo hautainufaisha tu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), bali pia utachochea kuboresha maisha ya wananchi.

Bw. Manzi Rwegasira, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, alielezea kuwa mkataba huo ni hatua muhimu katika kudhihirisha dhamira thabiti ya benki hiyo ya kuunga mkono ustawi wa Zanzibar na maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa ujumla.
Katika kuthibitisha azma hiyo, Rwegasira alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, Stanbic imefanikisha kupatikana kwa zaidi ya dola bilioni 1 za Marekani (sawa na takriban Sh trilioni 2.6) kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akisisitiza umuhimu wa ukopeshaji wa pamoja, kiongozi huyo alieleza kuwa mkopo huu utawezesha utekelezaji wa miradi muhimu ya kijamii na kiuchumi, ambayo itakuwa na athari chanya za moja kwa moja kwa maisha ya watu wengi na kuchochea maendeleo endelevu ya Zanzibar.
“Sisi, kama benki ya Stanbic, tuna dhamira ya dhati ya kuchangia maendeleo ya Tanzania kwa sababu hapa ni nyumbani kwetu. Tunawajibika kuwa sehemu ya ukuaji wa taifa letu kwa kuhakikisha upatikanaji wa ufadhili wa kimkakati kama huu tulioshirikiana na PBZ.”
Bw. Rwegasira alisema kuwa mkopo huu ni zaidi ya mtaji na utazinufaisha sekta kuu kama vile uvuvi, uchukuzi wa baharini, nishati, utalii, na miundombinu, huku uchumi wa buluu ukinufaika kwa njia nyingi na katika namna tofauti.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya PBZ, Arafat Ally Haji, alieleza kuwa mkopo huu wa maendeleo utasaidia miradi mikubwa ya kimkakati na miundombinu ya serikali, ikiwemo uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Zanzibar.
Alisema kuwa mkopo wa pamoja una lengo la kuharakisha mwelekeo wa ukuaji wa Zanzibar na kuimarisha maendeleo yake kwa ujumla kwa kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.
“Fedha hizi zitawezesha kukamilika kwa miradi ya kijamii na kiuchumi inayoendelea, huku pia zikifadhili mipango mipya inayopangwa na mamlakaili kuhakikisha ustawi wa kudumu kwa wananchi wa Zanzibar,” alisema Haji.



