Sefue ataja mafanikio Tume Haki Jinai

DODOMA – KAMATI ya kuandaa mkakati wa kutekeleza Tume ya Haki Jinai, imekabidhi mkakati wa kutekeleza mapendekezo ya tume huku ikibainisha mafanikio kadhaa yaliyopatikana.

Akiwasilisha taarifa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan jana Ikulu ya Chamwino, Makamu Mwenyekiti wa kamati, Balozi Ombeni Sefue alisema mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi kutoa waraka namba 1 wa mwaka 2023 unaowaelekeza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuzingatia ipasavyo matumizi sahihi ya sheria inayowapa mamalaka ya ukamataji.

Alisema waraka huo unalenga kutafuta dawa ya malalamiko ya wananchi kuwa wakati mwingine mamlaka haya yanatumika vibaya kinyume na lengo na kinyume na sheria.

“Waraka huo pia umebainisha kuwa iwapo mwathirika wa maamuzi ya kukamatwa atafungua shauri mahakamani na ikibainika kiongozi alikiuka sheria wakati wa kukamata, kiongozi huyo atawajibika yeye mwenyewe na serikali haitakuwa sehemu ya shauri litakalotokana na ukiukwaji huo wa sheria,” alisema.

Balozi Sefue alisema mifumo ya Tehama imeunganishwa katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mahakama na Jeshi la Polisi hatua ambayo imeongeza ufanisi na uwazi katika kushughulikia makosa ya jinai.

Ofisi ya Taifa ya Mashitaka

Alisema hadi Juni 7 mwaka huu, majalada 18, 996 kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka yametumwa kwenda mfumo wa mahakama.

Alisema pia ofisi hiyo imefungua ofisi katika wilaya 50 kati ya wilaya 96 ambazo hazikuwa na ofisi. Alisema Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya tasnia ya sheria namba 8 B imerekebishwa ili kuondoa changamoto katika kupokea ushahidi wa mtoto.

Balozi Sefue alisema pia jaji mkuu ametoa kanuni zinazoongoza uchukuaji wa maelezo ya watuhumiwa kwa njia ya kieletroniki. Alisema mahakama imekamilisha mfumo wa usimamizi wa mashauri ambao utawezesha upatikanaji wa nakala ya mwenendo wa mashauri na hukumu.

Alisema ili kufanya Jeshi la Magereza kutokuwa sehemu ya kuadhibu pekee bali pia kurekebisha tabia za wafungwa , jeshi hilo limeongeza matumizi ya maofisa magereza kutoka 238 waliokuwapo Julai mwaka jana hadi 339 ilipofika Juni 2024.

Alisema pia zimeanza kutumika kanuni za maadili za waendesha mashtaka na ofisi ya waendesha mashtaka imewezeshwa kifedha na kuondoa changamoto ya malipo ya mashahidi kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Kuhusu mambo yaliyokamilishwa na kamati, Balozi Sefue alisema ni mkakati wa utekelezaji wa mapendekezo ya tume ambao umebainisha afua zitakazotekelezwa na taasisi zenye wajibu wa kutekeleza, gharama za utekelezaji na viashiria vya ufuatiliaji na tathmini vitakavyosaidia kupima matokeo ya utekelezaji wa mapendekezo ya tume.

SOMA: Serikali: Tutazingatia maoni kanuni za uchaguzi

Alisema pia kamati imeandaa mkakati wa upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharimia shughuli za haki jinai na mkakati wa mawasiliano wa haki jinai.

Aidha, Balozi Sefue alisema mambo ambayo hajakamilika ni pamoja na mkakati kubaini uhalifu lengo likiwa ni kuweka mifumo imara ya kubaini na kuzuia uhalifu, kuunganisha na kuimarisha mifumo ya utambuzi wa watu, usajili wa mali, urasimishaji , ufungamanishaji wa biashara na huhuma za kijamii.

Mengine ni uboreshaji wa sheria 11 zinazohusu masuala mbalimbali ikiwamo menejimenti ya vielelezo na makosa ya uhujumu uchumi. Alisema pia uanzishwaji wa ofisi ya upelelezi na kuboresha muundo, ujenzi ya ofisi na makazi kwa watumishi wa taasisi za haki jinai.

Kuhusu mapendekezo, Balozi Sefue alisema kamati imependekeza wakati wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala serikali ihakikishe taasisi zote za haki jina zinakuwa na majengo ya kutosha.

Habari Zifananazo

Back to top button