Serikali: Tutazingatia maoni kanuni za uchaguzi

DODOMA – Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Zainab Katimba amesema maoni ya vyama vya siasa ni muhimu hivyo yatazingatiwa katika kuboresha kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Katimba amesema hayo leo wakati akifungua kikao cha wadau kutoka katika vyama vya siasa, kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa lengo la kujadili rasimu ya kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024.

“Maoni ya vyama vya siasa ni muhimu sana ili kuboresha kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 ambazo zimeandaliwa na kuletwa kwenu ili mtoe maoni ya kuziboresha,” amesema Katimba.

Kanuni zimeandaliwa kwa kuzingatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anataka uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 uwe huru na wa haki.

Katimba ameainisha kuwa, Kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa uandaliwa ili kukidhi matakwa ya kifungu 201 (A) cha sheria ya serikali za mitaa (mamlaka za wilaya) sura 287 na kifungu 87 (A) cha sheria ya serikali za mitaa (mamlaka za miji) sura 288 vinavyomtaka waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kuweka utaratibu wa uchaguzi wa serikali za mitaa kupitia kanuni.

SOMA: Mfahamu msemaji mkuu mpya wa serikali

Ameitaja kanuni ya kwanza iliyoandaliwa kuwa ni kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za wilaya za mwaka 2024.

Sanjari na kanuni hiyo, Naibu Waziri ameeleza kanuni nyingine zilizoandaliwa ambazo ni za uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa katika mamlaka za miji za mwaka 2024, za uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji za mwaka 2024 na za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo za mwaka 2024.

Katimba amewasisitiza washiriki wote kutoa maoni yanayolenga kuziboresha kanuni hizo na kuongeza kuwa, ana imani kwamba watashiriki kikamilifu kutoa maoni yenye tija na maslahi kwa taifa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button