Mfahamu msemaji mkuu mpya wa serikali

DODOMA – Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi kadhaa jioni ya leo Juni 15, miongoni mwa teuzi hizo ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Thobias Makoba anachukua mikoba ya Mobhare Matinyi ambaye amepangiwa majukumu mengine kwa mujibu wa taarifa ya kurugenzi ya mawasiliano ya Rais- Ikulu.

Makoba amewahi kufanya kazi kama Msaidizi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, marehemu Bernard Membe na kwa sasa alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Wengine walioteuliwa ni pamoja na Afisa Mwandamizi Ofisi ya Rais – Balozi John Simbachawene, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara.

SOMA: Nape: Tanzania kinara ubora kidijiti duniani

Pia, Bw. Nkoba Mabula aliyekuwa Afisa Mwandamizi Ofisi ya Rais – Ikulu ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii. CP Benedict Wakulyamba amepangiwa kushughulikia Maliasili katika Wizara hiyo kwa nafasi yake kama Naibu Katibu Mkuu.

Taarifa ya Ikulu imesema, Rais Samia amemteua Dk Habib Kambanga kuwa Balozi. Kambanga alikuwa Afisa Mwandamizi Ofisi ya Rais Ikulu.

Vilevile, Rais Samia amemteua Afisa Tawala Mwandamizi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Bukombe, Bw. Rajab Mketo kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe. Bw. Mketo anachukua nafasi ya Onesmo Kisoka ambaye amestaafu.

Uteuzi mwingine ni wa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dk Mary Levira, ambaye kateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. 

Habari Zifananazo

Back to top button