Nape: Tanzania kinara ubora kidijiti duniani

GENEVA, Uswisi – WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amethibitisha nia ya Tanzania kuwa kinara wa ubora wa kidijiti Afrika na kote duniani.

Aliyasema hayo akihutubia katika Siku ya Bunifu za Kidijiti Duniani, Geneva, Uswisi wakati wa tukio la kwanza la Siku ya Bunifu Dunia ya Kidijiti lililoandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Tukio hilo linakusudia kuonesha nguvu ya bunifu za teknolojia za kidijiti kuendesha ubunifu, kuunganisha watu na kuleta maendeleo endelevu duniani.

Katika tukio hilo alisema Tanzania haithamini tu ulimwengu wa kidijiti na teknolojia za kidijiti, bali pia inaongoza mpango wa ubunifu katika sekta mbalimbali ili kutumia teknolojia kwa mabadiliko chanya na maendeleo.

Miongoni mwa mipango ya ubunifu iliyotajwa na Nape ni uwekezaji wa Tanzania katika teknolojia za elimu, maendeleo ya miji ya kisasa, ubunifu katika kilimo, hatua za usalama wa mtandao na benki mtandao.

Alisisitiza umuhimu wa Serikali ya Tanzania kuhifadhi haki za ulinzi wa taarifa binafsi na faragha huku ikikuza utamaduni wa kuendeleza ubunifu wa kidijiti.

SOMA: Tanzania kidedea Mashindano ya TEHAMA China

“Kwa kuweka mazingira ya kisheria yanayounga mkono viwango vya kimaadili na haki za watumiaji, Tanzania inajiweka kama kinara wa ubora wa kidijiti Afrika,” aliongeza Nape.

Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania UN, Geneva, Dk Abdullah Possi, ambaye pia anawakilisha nchi katika ITU, alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa Tanzania katika michakato ya sera za kimataifa zinazohusiana na teknolojia za kidijiti.

Habari Zifananazo

Back to top button