Serikali yafunga kambi ya Nduta, yahimiza amani
KIGOMA; SERIKALI ya Tanzani imeifunga rasmi kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma, iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi.
Hatua ya kufunga kambi hiyo imekuja baada ya wakimbizi zaidi ya 166,000 waliokuwa wakihifadhiwa kwenye kambi hiyo kurudishwa nchini mwao, huku Waziri wa mambo ya Ndani, Patrobas Katambi akihimiza umuhimu wa kutunza amani ya Tanzania.
Akizungumza katika hafla ya kufungwa kambi hiyo leo Aprili 30, 2026, Waziri Katambi amesema uwepo wa wakimbizi wa Burundi waliokuwa wakihifadhiwa kwwenye kambi hiyo ni mfano dhahiri wa kuvurugika amani nchini mwao, hivyo hawakuwa na chaguo lingine zaidi ya kuomba hifadhi Tanzania.

Ametoa wito kwa Watanzania kulinda na kudumisha amani,kwani ni muhimu na ikitoweka itasababisha shughuli zote za maendeleo na mambo muhimu ambayo Watanzania walijipangia hayatafanyika.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Naibu Mkuu wa UNHCR nchini, Zulqarnain Hussain, ameishukuru Tanzania kwa moyo wake wa ukarimu wa kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi hao, ambao waliishi kwa amani muda wote.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Sudi Mwakibasi alisema Tanzania ilianza kuhifadhi wakimbizi wa Burundi katika kambi hiyo mwaka 2016, wakipokea wakimbizi 125,000 na hadi kambi inafungwa jumla ya wakimbizi zaidi ya 166,330 walikuwa wamerejeshwa Burundi.



