BAADHI ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika sekondari ya Mustafa Sabodo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara wameipongeza serikali kwa kuwajengea madarasa yaliyogharimu Sh milioni 58.
Pongezi hizo zimetolewa leo wakati Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Stergomena Tax alipozindua mradi wa ujenzi wa madarasa shuleni hapo.
Mwanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo, Roswita Fulbert amesema ujenzi huo utawasaidia kuongeza bidii katika kujifunza shuleni hapo kwa wanafunzi waliyopo na wengine watakaokuja.
“Kabla ya kuongeza kwa haya madarasa tulikuwa tunapitia changamoto ya uchache wa madarasa na wanafunzi tuko wengi kwahiyo uwepo wa mradi huu ni furaha kubwa sana kwetu sisi wanafunzi”amesema Roswita
Mwanafunzi wa kidato hicho cha nne shuleni hapo, Anafi Hassan “Mradi huu utatunufaisha sana sisi wanafunzi na tutapata elimu bora na kwa wakati, kabla ya huu ujenzi tulikuwa tunakaa wanafunzi wengi darasa moja ila sasa hili tatizo limeisha”
SOMA: Sh bilioni 52 zatumika ujenzi shule za msingi, sekondari …
Amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuona umuhimu wa elimu hivyo asiishie tu hapo bali aendeleze jitihada hizo.
Mwalimu mkuu shuleni hapo, Haji Nyengedi amesema ujenzi huo umehusisha matundu sita ya vyoo, madara mawili pamoja na ofisi moja huku idadi ya wanafunzi shuleni ikiwa ni zaidi ya 900.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Selemani Nampanye amezungumzia changamoto ya uzio inayoikabili shule hiyo hivyo ameiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto hiyo kwa ajili ya usalama wa wanafunzi hao.
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi, amewasisitiza wanafunzi hao kuwa elimu ni kitu cha muhimu kwani bila elimu hawawezi kuendelea.
“Juhudi hizi zitakuwa ni bure wanafunzi, wanangu kama hamtatumia fursa hii mliyoipata kwa kujiendelea kusoma kwa bidii katika mazingira mazuri”
Ameongeza kuwa, “Baada ya hapo kuelimika na kuitumia fursa hii itawafungulia milango ya maisha katika maeneo mbalimbali”amesema Tax
Aidha Waziri huyo yuko katika ziara ya kikazi ya siku tano mkoani humo kuanzia leo Oktoba 6, mwaka huu kwa ajili ya kuzinduza na kuweka jiwe la msingi miradi mbalimbali ya maendeleo lakini pia amepata fursa ya kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo.