Sekta 8 uchumi wa buluu zapaa

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi.

SEKTA kuu nane za uchumi wa buluu zimepata mafanikio makubwa katika miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuinua na kuongeza fedha za kigeni katika mapato ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema hayo jana visiwani humo katika Hotuba yake aliyoitoa katika maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi.

Alizitaja sekta hizo kuu nane za uchumi wa buluu zenye mafanikio kuwa ni pamoja na uvuvi na ufugaji wa mazao ya baharini, ukulima wa mwani, utalii, bandari na biashara za usafiri wa majini, mafuta na gesi asilia.

Advertisement

Alisema katika utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu, serikali imeimarisha sekta ya uvuvi na ukulima wa mazao ya baharini ili kuongeza tija katika shughuli hizo na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Dk mwinyi alisema serikali imewapa wananchi mbinu bora za kutekeleza shughuli zao, vifaa vya kufanyia kazi pamoja na ujenzi wa madiko na masoko ya kuuzia samaki ili wawe na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Katika eneo hilo boti 1,027 za uvuvi na kilimo cha mwani zimetolewa na kuwanufaisha wananchi 32,000  ambao kati yao, asilimia 70 ni vijana. Asilimia 90 ya boti za ukulima wa mwani wanufaika wake ni wanawake.

Katika kuimarisha miundombinu ya uvuvi, alisema serikali imekamilisha ujenzi wa diko la samaki la kisasa la Malindi ambalo limeanza kutumika likihudumia wastani wa watu 10,000 na boti za uvuvi 350 kwa siku.

Alieleza mafanikio mengine ni serikali kuendelea na ujenzi wa viwanda vya kuongezea thamani dagaa eneo la Kama-Unguja na Ndagoni-Pemba sambamba na matayarisho ya ujenzi wa bandari mbili za uvuvi.

Bandari hizo zipo katika eneo la Ngalawa Unguja na Shumba Mjini kwa Pemba pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki katika eneo la Fungurefu Mkoa wa Kaskazini Unguja.

“Kwa jitihada hizo za serikali zimechochea uzalishaji wa samaki wanaovuliwa kwa asilimia 107.2 kutoka tani 38,107 mwaka 2020 zenye thamani ya Shilingi bilioni 205.35 hadi kufikia tani 78,943 mwaka 2024 zenye thamani ya Shilingi bilioni 618.18,” alisema.

Kwa upande wa kilimo cha mwani, alisema jitihada zilizofanywa ni kuimarisha ukulima wa zao hilo kwa kuwapa wakulima vifaa, taaluma na kuwajengea mazingira bora ili wapate mafanikio.

Alisema ujenzi wa kiwanda cha kusarifu mwani kilichopo Chamanangwe Pemba umekamilika na kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 30,000 za mwani mkavu kwa mwaka na kitakapoanza kazi, kitachochea uzalishaji wa zao hilo na kuwa na soko la uhakika.

Alisema kwa wastani ukulima wa mwani unatoa ajira kwa watu 16,000 na asilimia 80 ya wakulima wa zao hilo ni wanawake.

Katika sekta ya utalii, Dk Mwinyi alisema katika miaka 61 ya Mapinduzi, mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta hiyo kwa kuongezeka kwa idadi ya watalii na kuimarika kwa sekta ya huduma.

Alisema idadi ya watalii walioingia imeongezeka kutoka 568,312 Novemba 2023 hadi 645,144 Novemba 2024 sawa na ongezeko la asilimia 14.