Sensa: Vyombo vya majini vyafikia 52,189

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wametoa ripoti ya sensa ya vyombo vidogo vya usafiri majini vinavyopatikana eneo la Tanzania bara, ambayo imebainisha kuwepo kwa jumla ya vyombo 52,189.

Akizindua ripoti hiyo Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete alisema ripoti hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi hasa katika kuchochea uchumi wa buluu, kutengeneza ajira na kupunguza umaskini wa kipato.

Mwakibete aliongeza kuwa sensa hiyo itumike kuboresha mipango katika sekta ya uvuvi pia sera na kanuni zitakazosimamia usalama wa vyombo vinavyosafiri kwenye maji.

“Mojawapo ya kilio kikubwa cha wavuvi ni wenzao wanapotea na taarifa hawapati na hawajui chombo chao kimeelekea mwelekeo gani lakini hii ni kutokana tulikuwa hatujafanya zoezi kama hili kutambua kwamba ni chombo gani kinahimili katika ziwa gani na bahari upande gani sababu vyote hivi vinatofautiana uwezo” alisema Mwakibete.

Aidha, ameshauri umuhimu wa ripoti hiyo kutafsiriwa kwa lugha ya kiswahili ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi huku akizitaka taasisi za elimu kutumia taarifa hizo kwa mafunzo na kuibua maeneo mengine ya utafiti yatakayoboresha shughuli zinazofanyika majini ikiwemo usafirishaji na uvuvi.

Awali akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Abdi Mkeyenge alisema kupitia taarifa hizo imeundwa kanzidata yenye taarifa muhimu za vyombo vidogo vya majini nchini ikiwemo aina ya chombo, matumizi yake, taarifa ya umiliki na aina ya nyenzo zinazotumika katika mawasiliano na uokozi, takwimu ambazo zimepangwa kwa ngazi ya kitaifa, kimkoa na kiwilaya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Nahodha Muna Mandia alisema sensa hiyo  imefungua fursa kwa taasisi za serikali zinazosimamia sekta ya majini kushirikiana katika usimamizi wa masuala ya kijamii na kiuchumi zinazotegemea usafiri wa vyombo vidogo vya majini.

“Sensa hii ni ya kwanza kufanyika nchini, katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hata pia katika nchi za jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) haijawahi kufanyika sensa kama hii” aliongeza Nahodha Mandia.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa vyombo 24,667 sawa na asilimia 53.65 vipo Ziwa Victoria , 6,615 (13.41%) vipo ukanda wa pwani ya bahari ya hindi, Ziwa Tanganyika ni 4,727 (10.28%) , Ziwa Nyasa ni 3,515 (7.65%) na maeneo mengine ya maji ikiwemo mito na mabwawa ni 6,902 (15.01%) huku kigezo kilichotumika kuvihesabu ni vyenye ukubwa kuanzia mita nne na kuendelea.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button