Serengeti Girls leo ndio leo

TIMU ya soka ya taifa ya wasichana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Girls, leo itakuwa na kibarua cha kutafuta ushindi dhidi ya Canada ili kujihakikishia kufuzu robo fainali ya Kombe la Dunia.

Mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi utachezwa kwenye Uwanja wa DY Patil mjini hapa kuanzia saa 20:00 usiku ambapo kwa nyumbani itakuwa saa 10:30 jioni.

Aidha, kuepuka kupanga matokeo mechi zote za Kundi D zitachezwa muda mmoja, ambapo vinara Japan wenye pointi sita watakuwa wakikipiga na Ufaransa katika Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru, Goa.

Akizungumza na gazeti hili kocha wa Serengeti Girls, Bakari Shime alisema kwa jinsi wachezaji walivyo na ari, anaamini watashinda mchezo huo na kuendelea kuonesha ulimwengu kuwa kuna nchi inaitwa Tanzania kwenye ramani ya soka kama walivyowashangaza Ufaransa au Les Bleuettes.

“Kwa jinsi tulivyojiandaa wachezaji wana hamu na nia ya kushinda mchezo wa kesho (leo). Tumejiandaa vema kisaikolojia na kimbinu, najua Canada watakuja kwa nia ya kushambulia ili wapate bao kwa sababu hawana cha kupoteza ila na mimi nimewaandaa wachezaji kuibeba mechi na kuhakikisha wanashinda,” alisema Shime.

Alisema wao kwa matokeo yoyote ya ushindi au sare itawapeleka robo fainali na wachezaji wake wanaonesha wanahitaji kufuzu kutokana na mazoezi waliyofanya baada ya kuwasili Mumbai.

Katika mchezo wa leo wachezaji Neema Paul na Joyce Lema watakosekana kwa sababu wanatumikia adhabu ya kadi nyekundu walizooneshwa katika michezo iliyopita.

Mechi nyingine zitakazochezwa leo mchana, Colombia wataivaa Mexico huko Goa na China itacheza na bingwa mtetezi, Hispania kutoka Kundi C.

Matokeo ya mwisho ya mechi za leo kwa Kundi C ndiyo yatakayoamua timu mbili zitakazofuzu robo fainali kwa sababu kila moja ina pointi tatu.

Kundi A na B ilitarajiwa kumaliza michezo yao jana, ambapo kinara wa Kundi A, Marekani (pointi nne) walicheza na Morocco yenye pointi tatu na Brazil yenye pointi tatu dhidi ya wenyeji India ambao hawana kitu.

Kundi B, New Zealand ambayo haina pointi dhidi ya kinara Ujerumani  yenye pointi sita na Nigeria yenye pointi tatu inaivaa Chile yenye pointi tatu wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button