Serengeti girls mguu sawa India

TIMU ya Taifa ya soka ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls, inatarajia kuondoka leo hapa kwenda India kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kuanza Oktoba 11-31 mwaka huu.

Serengeti Girls walikuwa wameweka kambi Southampton, Uingereza kuanzia Septemba 26 wamefanya mazoezi na kucheza michezo miwili ya kirafiki.

Akizungumza na gazeti hili Kocha mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime alisema kambi hiyo imewawezesha kufanya mazoezi vizuri na wanaonekana wamechangamka.

“Tumepata vitu vingi vizuri na vipindi kadhaa vya mazoezi na kucheza michezo miwili ya kirafiki, lakini imekuwa kambi yenye faida, kwani wachezaji wamechangamka kutokana na utulivu waliopata,” alisema.

Alisema awali programu hii ilikuwa ikamalizikie Dubai kwa kucheza michezo mitatu ya kirafiki na timu ambazo zinashiriki Kombe la Dunia lakini kambi ya Uingereza ilichelewa, hivyo nafasi imekuwa finyu ya kupata mechi zaidi za kirafiki.

Alisema amepata picha halisi ya kikosi chake na mchezo wa kwanza dhidi ya Japan utakaochezwa Oktoba 12 katika Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru uliopo Goa watapata ushindi. Baada ya mchezo huo, Serengeti Girls watashuka tena katika dimba hilohilo kuwavaa mabingwa watetezi, Ufaransa Oktoba 15 na mchezo wa mwisho katika makundi watacheza na Canada Oktoba 18 katika Uwanja wa DY Patil uliopo Nerul, Navi Mumbai.

Serengeti Girls ambao walikuwa wageni wa timu ya Southampton ambayo ipo kilometa 128 kutoka London, walicheza michezo miwili na timu za wanawake za klabu hiyo na kushinda mmoja na mwingine walitoka sare ya bila kufungana.

Juzi walitembelea Jiji la London na kufika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini hapa kabla ya kutembelea kasri la kifalme Holyroodhouse huko Edinburgh, Scotland na kupiga picha za kumbukumbu.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x