Serikali imefuta tozo 374 kwa wawekezaji

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Stanslaus Nyongo amesema kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, serikali imefuta tozo 374 ili kuondoa kero kwa wawekezaji.
Mbali na tozo, amesema baadhi ya sheria pia zimefutwa na nyingine kurekebishwa zikiwemo sheria 62, na hivyo kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
Nyongo ameyasema hayo leo wakati wa mwendelezo wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Tanga, ambapo Rais amefanya ufunguzi rasmi wa mradi wa awamu ya pili ya kiwanda cha chokaa na saruji (Maweni Limestone) kilichopo wilayani Tanga.
Ameongeza kuwa katika mkutano wa bunge uliopita, imepitishwa sheria ya kuunganisha taasisi mbili za TIC na EPZA zinazowahudumia wawekezaji wa nje na ndani ili kuanzisha mamlaka ya kushughulikia wawekezaji.
Sheria hiyo pia itaruhusu kuanzisha kituo maalumu cha kukaribisha wawekezaji kwa maana ya usajili na kuwatambua kama wawekezaji wa kimkakati.
Vile vile sheria hiyo imelenga kuanzisha benki ya ardhi ili wawekezaji wanapokuja Tanzania wakute sehemu ambazo zipo tayari kwa ajili ya uwekezaji.



