‘Serikali inatambua umuhimu ushirikiano Sekta ya Umma, Binafsi’
SERIKALI imesema inatambua umuhimu wa ushirikino kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika kukuza uchumi wa nchi, huku ikiahidi kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuleta maendeleo ya nchi.
Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), kutoka Wizara ya Fedha, Bashiru Taratibu amesema hayo wakati akifunga mafunzo kuhusu dhana ya PPP, Sheria ya PPP Sura 103 pamoja na Sera ya Taifa ya PPP, kwa maafisa bajeti wa Wizara hiyo yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Ametoa wito kwa Sekta Binafsi kuendelea kuungana na Serikali katika juhudi zake za kuhakikisha kuwa uchumi unaendelea kukua, huku wananchi wakipata huduma zote muhimu ikiwemo huduma za Afya, maji, elimu pamoja na huduma nyingine.

‘’Nchi nyingi wanatumia utaratibu huu kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuishirikisha sekta binafsi ambayo kwa kiasi kikubwa tunaitaka ije iungane na Serikali kutoa huduma zile ambazo Serikali imekuwa ikizitoa’’ amesema Taratibu.
Ameongeza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha watumishi hao wa Wizara ya Fedha wanakuwa na ujuzi wa kutosha katika masuala ya ubia kati ya Sekta hizo kwa kuwa ni miongoni mwa watendaji muhimu katika masuala ya bajeti ili kukuza uchumi wa nchi.
‘’Tumewaleta kwenye kozi hii ili muweze kutoa ushirikiano kuhakikisha kuwa tunatengeza nguvu ya pamoja ili pale ambapo kunakuwa na mradi wa kufanya basi mnakuwa na uelewa wa nini mnachotakiwa kufanya kama wajumbe wa PPP, Wizara ya Fedha, ili tuweze kuchambua na kumshauri Mhe. Waziri wa Fedha,’’ Amesema.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Afisa Bajeti wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Wizara ya Fedha, ambaye pia ni Mwenyekiti wa mafunzo, Tumwesige Kazaura, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa na ufahamu juu ya umuhimu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

‘’Kwakweli kupitia mafunzo haya, tumeweza kutambua kazi kubwa ambayo inafanywa na Wizara, kwa hiyo yale maswali ya mbona hatuoni miradi ya PPP hatutarajii kuyasikia kutoka kwa wataalam hawa, sanasana sisi ndio tutakuwa mabalozi wa kuwajibu wataalam wengine nje ya wizara’’ amesema Kazaura.
Kwa upande wake Afisa Bajeti wa Idara ya Huduma za Sheria, Wizara ya Fedha, Angelina Chilewa, ameipongeza wizara, kupitia Kitengo cha PPP, kwa kuwaandalia mafuzo hayo muhimu huku akiahidi kuendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

‘’Tunashukuru sana kwa mafunzo haya na tunaahidi kuwa mabalozi tunapokwenda kwenye Ofisi zetu na hata jamii, kubadili mitazamo yao kujua faida ambazo Serikali inaweza kupata kupitia miradi ya PPP’’ amesema Chilewa.
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau, ipo katika hatua za utekelezaji wa Sera ya Taifa ya PPP pamoja na Sheria ya PPP, Sura 103.



