Serikali kufanya sensa ya uzalishaji viwandani

SERIKALI imetangaza kuanza kwa Sensa ya Uzalishaji Viwandani mwaka huu, ikiwa ni mara ya tano kufanyika nchini tangu kuanzishwa kwake.
Sensa hiyo, inayotekelezwa kwa mara ya kwanza kwa pamoja Tanzania Bara na Zanzibar, inalenga kutoa takwimu sahihi zitakazosaidia kubaini mwenendo wa sekta ya viwanda, changamoto zake, na mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, amesema kuwa sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 2013, na sasa ni wakati mwafaka wa kupata takwimu mpya kwa ajili ya kupanga maendeleo ya sekta ya viwanda.
“Takwimu ni msingi wa maamuzi bora. Kupitia sensa hii, tutajua hali ya viwanda vyetu, mchango wake katika Pato la Taifa, na nini kifanyike kuinua sekta hii,” amesema Waziri Jafo.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Amina Msengwa, amesema kuwa wadadisi 246 kutoka mikoa yote Tanzania Bara wamepewa mafunzo ya siku 12 ya nadharia na vitendo mjini Iringa chini ya wakufunzi 47 ili kuhakikisha ukusanyaji wa takwimu unafanyika kwa ufanisi mkubwa.
“Sensa hii ni muhimu na kwa kweli haihitaji kusubiri miaka 10, tutaifanya kwa kutumia teknolojia za kisasa kuwezesha kupata takwimu sahihi zaidi. Tunahitaji data za mara kwa mara ili kujibu masuala ya maendeleo ya Taifa,” amefafanua Dk Msengwa.
Kwa mujibu wa Dk Msengwa, sensa hii itakusanya taarifa muhimu kama uanachama, usajili wa viwanda, udhibiti wa ubora na utafiti na maendeleo.

Zingine ni taarifa za masoko, usimamizi wa mazingira, aina ya teknolojia ya mitambo inayotumika, na mipango ya kuendeleza uwekezaji pamoja na changamoto zinazoikabili sekta hii.
Kwa niaba yake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, amesema kuwa takwimu za viwanda ni muhimu katika kuonyesha mwelekeo wa uchumi wa Taifa na mchango wa sekta hiyo kwenye maendeleo.
“Kama maamuzi yetu hayana namba, matokeo yetu hayatakuwa sahihi. Kupitia sensa hii, tutajua tumewekeza wapi na wapi tunapaswa kuboresha ili kuimarisha viwanda,” amesema James.
Akingumzia kwa kina umuhimu wa sekta ya viwanda, Waziri Dk Jafo alisema; “Sekta hii inategemea sekta nyingine kama miundombinu, umeme, maji na afya ili kuweza kukua kwa kasi.”
Alisema viwanda haviwezi kusimama peke yake bila uwekezaji katika huduma muhimu na akaipongeza serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika maeneo yote yanayofanya shughuli za viwanda kukua.
“Sensa hii itasaidia kubaini nafasi ya Tanzania katika ushindani wa viwanda Afrika. “Mwaka 2013, tulikuwa na viwanda 49,273. Sasa tunakwenda kupata takwimu zitakazotufanya tuone tumepiga hatua kiasi gani na jinsi tunavyoweza kushindana na mataifa mengine ya Afrika,” amesema.

Aidha, Waziri Jafo amesisitiza kuwa takwimu za viwanda ni msingi wa kupanga sera na mikakati ya maendeleo.
Waziri Jafo pia ameweka msisitizo kuhusu umuhimu wa amani katika maendeleo ya viwanda na sekta nyinginezo.
Ameeleza kuwa miradi mikubwa kama barabara, reli, umeme na viwanda vimefanikiwa kwa sababu ya utulivu wa kisiasa nchini.
“Leo hii mtu anaweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mpanda au Sumbawanga bila matatizo, tofauti na zamani ambapo mtu alifika akiwa amejawa vumbi. Hii ni matokeo ya amani na maendeleo,” amesema.
Ameeleza kuwa nchi nyingi zilizoathirika na migogoro, kama Libya na Palestina, zimepoteza uthabiti wao wa kiuchumi kutokana na kukosa amani.
“Na sisi tunafahamu, Tanzania ina maadui wa ndani na nje, lakini tusiruhusu watu waangamize utulivu wetu. Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika sekta mbalimbali, na yote haya yamewezekana kwa sababu ya amani,” amesema.
Jafo pia amesisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika ajira, akisema kuwa zaidi ya wahitimu 60,000 wanamaliza vyuo vikuu kila mwaka, hivyo sekta ya viwanda inapaswa kuwa sehemu ya suluhisho la ajira nchini.
Kwa mujibu wa Jafo, wadadisi wa sensa wanapaswa kutekeleza kazi zao kwa uadilifu, kwani ni marufuku kuvujisha taarifa za viwanda binafsi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Daniel Masolwa, takwimu zote zitakusanywa kwa usahihi na kutolewa kwa pamoja ili kutoa picha halisi ya hali ya viwanda nchini.
Masolwa alisema serikali inatarajia kwamba matokeo ya sensa hii yatatoa mwongozo wa sera, mipango na maamuzi bora kwa mustakabali wa sekta ya viwanda, uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.



