Serikali kujenga Akademi za Michezo kikanda

DODOMA; SERIKALI imesema inaendelea na ujenzi wa Akademia ya Michezo yenye hadhi ya kimataifa Malya, wilayani Kwimba Mkoa wa Mwanza na mipango ni kujenga vituo hivyo kikanda.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma alipokwa akijibu swali la Mbunge wa Bumbuli, Ramadhan Singano, aliyehoji lini Serikali itaanzisha Kituo cha Michezo (Sports Academy) – Bumbuli kwa kuwa lipo eneo kubwa kwa ajili ya viwanja vya michezo.
“Kwa sasa tunaendelea na ujenzi wa Akademia ya Michezo yenye hadhi ya kimataifa Malya wilayani Kwimba Mkoa wa Mwanza chini ya Mkandarasi CRJE (East Africa) Limited, ambapo mpango wa serikali ni kujenga vituo hivi kikanda na tumeanza na Kanda ya Ziwa.
“Wakati serikali ikiwa inaendelea na juhudi hizo, nitoe rai kwa uongozi wa Halmashauri ya Bumbuli, kushirikiana na wadau wa michezo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kufadhili ujenzi wa kituo hicho muhimu kwa vijana wanamichezo wa Bumbuli,” amesema Naibu Waziri.
–



