Serikali kulipa fidia stahiki

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amewataka wananchi kuwa tayari kupisha miradi ya maendeleo inapopita katika maeneo yao na serikali italipa fidia stahiki.

Kutokana na azma ya kulipa fidia stahiki kulingana na thamani ya maeneo yatakayochukuliwa, tayari ameunda Tume ya Kupitia na Kutathmini masuala ya fidia katika utekelezaji wa miradi.

Aliyasema hayo alipofungua Barabara ya Juu ya urefu wa meta 231, Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.

SOMA: Mwinyi asisitiza ushirikiano utekelezaji miradi ya maendeleo

Dk Mwinyi alisema kaulimbiu ya uchaguzi waliyoitumia ya uongozi unaoacha alama inatekelezwa kwa vitendo.

Alisema katika kipindi cha awamu hii serikali imekusudia kuhakikisha inaacha alama kwa vizazi vijavyo kwa kutengeneza miundombinu imara itakayowasaidia wananchi wote, hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa jamii kutoa ushirikiano hasa kwa wale wanaopitiwa na miradi hiyo na wasiwe na wasiwasi wa kulipwa fidia zao kwani serikali haitamdhulumu mtu.

Sambamba na hayo, alieleza kuwa hayo ndiyo maendeleo endelevu ambayo huleta thamani katika kila kitu akitolea mfano sehemu inayopita barabara kila kitu kinakua kinapanda thamani kama vile ardhi, nyumba na hata shughuli za uchumi.

“Maendeleo ya kweli husababishwa na miundombinu nawaasa wananchi wawe tayari kupisha miradi ya maendeleo na serikali inalipa fidia stahiki na hakuna mtu atakayedhulumiwa na serikali, na ndiyo maana tumeunda tume ya kutathmini masuala haya ya madai kwa sababu maendeleo ni ya wote,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa kuna umuhimu wa kutunza miundombinu inayojengwa kwa kuhakikisha inabaki salama na kudumu kwa muda mrefu ili alama ionekane na inufaishe vizazi vijavyo.

Aliwataka wananchi kutojenga karibu na hifadhi ya barabara ili kuipa nafasi miundombinu mingine kama vile maji, umeme na intaneti.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohammed alisema miundombinu inayojengwa inatekelezwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) pamoja na maono na maelekezo ya Rais Mwinyi katika kutekeleza ilani pamoja na ahadi alizozitoa.

“Tunathibitisha kuwa maendeleo tunayoyaona yanatokana na maono yako na mipango yako katika kutimiza ahadi kwa wananchi wa Zanzibar na katika sekta yetu ya ujenzi barabara zote zimefumuliwa na zinajengwa katika ubora wa hali ya juu mijini na vijijini, hii ni alama kubwa uliyoiweka na haitofutika,” alisema.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ali Said Bakari alisema Barabara ya Juu hiyo ya meta 231 ya Mwanakwerekwe imejengwa na Kampuni ya CCECC kwa gharama ya Sh bilioni 23.7, ikiwa na uwezo wa kupitisha magari mawili kwa pamoja kwa kila njia moja.

“Ujenzi wa Barabara ya Juu ulianza rasmi Desemba Mosi, 2023 na ulikamilika Desemba 31, 2025 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 9.5 sawa na Sh bilioni 23.7 ambao umejumuisha nguzo za daraja, lampu, sakafu, barabara mbili, mzunguko wa njia, taa pamoja na alama za barabarani,” alisema.

Hii inakuwa barabara ya juu ya kwanza katika historia ya Zanzibar ambayo imepewa jina la Dk Hussein Ali Mwinyi na iko katika Barabara ya Mwanakwerekwe makutano ya njia inayotoka Amani, Fuoni, Mjini na Kwa Mchina Mombasa.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. l Get paid over $110 per hour working from home. l never thought I’d be able to do it but my buddy makes over $21269 a month doing this and she convinced me to try. The possibility with this is endless….

    This is what I do………………………………….. https://Www.Cash54.Com

  2. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→→→→→→→ https://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button