Serikali kushirikiana na sekta binafsi utoaji elimu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na sekta binafsi katika utoaji elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutosha unaohitajika katika sekta mbalimbali.

Waziri Majaliwa ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha malengo ya kukuza ujuzi na kuongeza soko la ajira yanafanikiwa kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.

Akizungumza Februari 24, 2023 katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uzalishaji wa rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira.

”Maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote yanategemea sana ngazi ya ujuzi wa nguvukazi uliyokuwa nayo. Hivyo, mchango wa wadau ni muhimu.”

Waziri Mkuu amewapongeza waajiri kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo (field practical), uanagenzi, utarajali pamoja na namna wanavyoshiriki wenu katika kuandaa mitaala inayotumika kwenye vyuo na taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu sana katika kuendeleza ujuzi kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda. “Nataka nitumie fursa hii kuwapongeza lakini Serikali inatambua na inathamini juhudi mnazozifanya katika utoaji wa ajira kwa wahitimu wetu, tunawapongeza sana.”

Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Uzalishaji wa Wafanyakazi Wenye Ujuzi Nchini Tanzania”, Waziri Mkuu amesema kauli hiyo ni thabiti kwani inaweka msisitizo katika ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Makakati wa Taifa wa Uendelezaji wa Ujuzi wa Mwaka 2016/17-2025/26 ambao moja ya malengo yake ni kuwa na ushirikiano kati ya waajiri, wadau na vyuo au taasisi za elimu.

Habari Zifananazo

Back to top button