Serikali kutoa mafunzo ya mtaala ulioboreshwa kwa walimu nchini

SERIKALI imesema itaendelea kutoa mafunzo ya mtaala uliboreshwa kwa walimu wote nchini ili kuhakikisha wanakuwa bora katika eneo la ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
Pia imewataka walimu wote waliopata mafunzo ya somo la elimu ya biashara nchi nzima kuwa na mtazamo mpya katika kufundisha somo hilo .
Naibu Katibu Mkuu Elimu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Atupele Mwambene amesema hayo wakati akimwakilisha Katibu Mkuu TAMISEMI, Adolf Nduguru kwenye ufungaji wa mafunzo ya walimu wa ajira mpya wa somo la Elimu ya Biashara katika mtaala ulioboreshwa yaliyofanyika Chuo cha Ualimu Korogwe mkoani Tanga.
Jumla ya walimu 1,913 wamepata mafunzo hayo katika Chuo cha Ualimu Tabora, walimu 513 Morogoro na 791 katika Chuo cha Ualimu Korogwe.
Mwambene amesema walimu wanapaswa kuwa na mtazamo chanya katika kufundisha somo hilo la elimu ya baishara kwa kuhakikisha wanafundisha vyema ili wanafunzi waweze kutumia somo hilo katika kujiajiri wenyewe.
“Mnaporejea katika vituo vyenu vya kazi haya mafunzo yakalete mabadiliko kwa wanafunzi nchini kwani maboresho katika mtaala umewekwa masuala ambayo yatamsaidia mwanafunzi katika kujifunza vyema suala la biashara,” amesema Mwambene.
Pia ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha elimu nchini ikiwemo kutoa ajira kwa walimu pamoja na kuidhinisha fedha za mafunzo kwa walimu wote na kuendelea kuimarisha sekta ya elimu.
Katika hatua nyingine, Mwambene ameitaka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuhakikisha inaendelea kuimarisha mafunzo endelevu kazini (MEWAKA) kwa walimu wote ili waweze kuendelea kujifunza katika jumuia za ujifunzaji kuongeza ujuzi na uelewa wa masomo wawapo kazini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba amewaasa walimu hao kuwa chanzo cha mabadiliko katika ufundishaji wao kwa somo hilo na kusema kuwa mbinu walizojengewa katika mafunzo hayo wazitumie vyema katika kuhakikisha wanakuwa bora.
“Hakikisheni mnazingatia yote mliyofundishwa kwenye mafunzo haya myatumie vyema mnaporejea katika vituo vyenu vya kazi , naomba sana mzingatie yote mliyofundishwa ili mkalete mabadiliko,”amesema, Dk Komba.
Naye, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Korogwe, Mary Mmari amesema mafunzo hayo yanatija kwa walimu wote walioweza kuyapata hivyo wakawe sehemu ya mabadiliko.
Mwakilishi wa Shirika lisilo la kiserekali la EDUCATE, Nelson Musikula amesema, kama wadau wataendelea kutoa ushirikiano katika kuinua elimu nchini hasa katika somo la elimu ya biashara ili kuwezesha wanafunzi wote nchini wanapata uelewa na kuweza kujifunza namna ya kuanzisha biashara.