Serikali kutokomeza changamoto watoto wa mitaani

MTWARA: WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk Doroth Gwajima amesema serikali inaendelea kuhakikisha inatokomeza changamato ya mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani katika maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yamejiri leo kwenye mdahalo ulioandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum uliofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani yatakayofanyika kitaifa Aprili 12, 2025 mkoani Mtwara.

Aidha amewataka wazazi wanapofikia hatua ya kuachana kuwatumia maofisa ustawi wa jamii ili  kukaa mezani na kupata muafaka wa malezi kwa watoto huku akiwataka wananchi kuwatumia vizuri maofisa maendeleo ya jamii ili kupata suluhisho la migogoro mbalimbali pale inapojitokeza kwenye familia.

Pia amewataka kutoa taarifa kwa maofisa hao ili waweze kutumia weledi wao kwa ajili ya kukabiliana na taarifa aliyoipokea kutoka kwa wananchi hao juu ya migogoro mbalimbali hasa pale inapokitokeza kwenye jamii hiyo ikiwemo talaka ambao umetajwa kuwa chanzo kikubwa cha watoto kwenda kuishi mtaani na wengine kufanyishwa kazi.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amesema Mkoa Mtwara huo una jumla ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani takribani 90 ambapo asilimia kubwa inaonyesha kuwa ni watoto wakiume ambapo takwimu hiyo ni ile ya watoto ambao tayari wameshafikiwa ingawa anaamini ya kuwa wapo watoto ambao hawajafikiwa na hawapo kwenye takwimu hiyo.

“Miongoni mwa changamoto inayopelekea uwepo wa watoto hao katika mkoa wetu ikiwemo kuwepo kwa talaka holela ambazo zimekuwa sababu kubwa ya watoto kukosa malezi yaliyo bora na baadhi ya watoto kupelekwa kwa bibi ambae nae anahitaji kuhudumiwa na baadhi ya familia kutoipa elimu kipaumbele,” amesema Sawala.

Hata hivyo katika kukabiliana na changamoto hiyo na kutambua umuhimu wa mtoto kwa mkoa na taifa kwa ujumla, mkoa umechukua hatua ikiwemo ya kuwaunganisha watoto kwenye huduma za marekebisho ya tabia, kuwapeleka kwenye vituo vya kulelea watoto pamoja na kuwaunganisha watoto na familia zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Saidi Nyengedi amesema uwepo wa watoto hao ni kosa la wazazi kwa kutozingatia umuhimu wa malezi kwa watoto hivyo wazazi watakapozingatia umuhimu wa malezi hakuna mtoto atakae ishi na kufanya kazi mtaa.

“Mimi nakataa wazazi wanaonyooshea vidole kwa kusema watoto wa sikuhizi, mimi nasema wazazi na walezi wasikuhizi ndio wenye matatizo mana wao wakichukua jukumu lao hapatakuwa na mtoto wa mtaani, mtoto aliyetelekezwa wala siyo unyanyasaji wa kijinsia ila tatizo tunalo sisi wazazi”amesema Nyengedi

Aidha kauli mbiu katika maadhimisho hayo ni ‘Imarisha Ushirikiano Kuzuia Watoto Kuishi Mtaani’

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button