Serikali kutumia ndege kuzuia uvuvi haramu
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) zinakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo ongezeko a plastiki baharini na uvuvi haramu ambapo wamejipanga kutumia teknolojia ya kisasa ili kukabiliana na adha hizo ikiwemo utumiaji wa ndege zisizo rubani ‘drones.
Akizungumza katika Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa OACPS unaoshirikisha nchi 78 kuangazia Sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu kuanzia leo Septemba 09-11 ambapo Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Serikali inaenda kutumia ndege zisizo na rubani ‘drones’ kufanya ‘survey’ ya kuangali maeneo yanaotumika zaidi kwa shughuli za uvuvi haramu ili kupata taarifa zitakazowasaidia wataalamu wetu katika operesheni tokomeza uvuvi haramu,” amesema Ulega.
Ulega amesema teknolojia hizi zinaenda kuwa na faida mbalimbali ikiwemo upataji wa habari za uhakika pia kuokoa fedha za serikali katika kutumia doria ‘patrol’ ambazo mara kadhaa hutokea kutobaini mahali sahihi panapofanyika uvuvi haramu.
Aidha, Ulega amezitaka Nchi Wanachama wa OACPS kuwajengea vijana uwezo ili kuwaongezea ushawishi katika kujifunza, kuzalisha na kusimamia rasilimali za bahari na uvuvi zitakazoimarisha Uchumi wa Buluu na kurithisha kizazi kimoja na kingine.
Kupitia Mkutano huo pia nchi Wanachama watajadili sera, kuelezea mafanikio na changamoto zake katika maendeleo ya sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki ikiwemo kubainisha na kuimarisha maeneo ya ushirikiano ya kimkakati kwa washirika mbalimbali wa maendeleo.
Amesema sekta ya uvuvi imekuwa chachu katika Uchumi wa Taifa ambapo kwa takwimu zilizopo nchini kwa sasa sekta hiyo huchangia asilimia 1.9 ya Pato la Taifa.
“Malengo yetu kufikia mwaka 2030 sekta ya uvuvi iongeze mchango wake katika Pato la Taifa kufikia asilimia 3 hadi 10,” amesema Ulega. SOMA : Ulega: Samia ameinua Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Mkutano huo pia umepangwa kufanyika sambamba na Kongamano la Kimataifa kuhusu Mikakati ya Uboreshaji wa Mnyororo wa Uzalishaji wa Vyakula vya Majini (Aquatic Food Value Chain) linaloandaliwa na Shirika ia Chakula Duniani (FAO)
SOMA: SERIKALI KUTUMIA NDEGE KUKAMATA WAVUVI HARAMU