Serikali kuwalinda watoto wanaotoa taarifa za ukatili

KAGERA: WANAFUNZI na watoto ambao wako chini ya umri wa miaka 18 wilayani Missenyi mkoani Kagera wamehakikishiwa kuwa siri zao wanazowasilisha katika madawati ya polisi na ustawi wa jamii kuhusu ukatili unaowakumba shuleni na majumbani zitalindwa hivyo wasiogope kutoa taarifa kwa vitisho wa waharifu.
Timu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) imekutana na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Minziro wilayani Missenyi yenye kidato cha kwanza hadi cha sita ambapoimetoa elimu ya kisheria kuhusu ukatili wa kijinsia na njia za kufikia mamlaka husika kuhakikisha changamoto zao zinasikilizwa na siri zinatunzwa na watuhumiwa kuchukuliwa hatua.

Grace Matofali kutoka Dawati la Jinsia Kitengo cha Polisi Missenyi ambaye pia ni miongoni mwa wataalamu wanaotoa Elimu ya msaada wa kisheria licha ya kutoa elimu kubwa juu ya madhara ya ukatili kwa jamii na changamoto zinazowakumba wanafunzi hao,pia amesema kuna wimbi la waharifu wanaotoa vitisho wa watoto wanaobakwa na kulawitiwa kuwa wakisemwa watauwa jambo ambalo linatia hofu watoto.
“Kwa upande wa polisi tunapokea kesi 5 au 6 za maswala ya ubakaji na ulawiti na kesi nyingine za vipigo ni nyingi sana zaidi ya hata 50 kwa mwezi , lakini kuna kundi la waharifu linalotisha watoto anambaka mtoto alafu anamwambia ukisema nitakuua, nitakunyonga, naomba niwahakikishie kuwa serikali imeweka ulinzi mkubwa kwa mtoto hivyo niwaondoe hofu,” amesema.

Hakika Ibrahim Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Missenyi amesema wilaya hiyo inapokea kati ya kesi 50 hadi 60 kwa mwezi juu ya maswala mchanganyiko ya ukatili kuhusu watoto na malalamiko mengi yakiwa ni utekelezaji wa watoto ,mimba, ubakaji na ulawiti jambo ambalo ni changamoto kwa watoto walioko chini ya miaka 18.

Amesema kwa sasa serikali imeweka mkazo sana na kushughulikia waharifu ambao wamekuwa wakitenda matukio ya ukatili kwa watoto wakiwemo wanafunzi ambapo hivi karibuni kuna baba wa mtoto amehukumiwa miaka 30 kwa kumpa mtoto wake mimba na akadai kuwa serikali ya Missenyi imefanikiwa kumrejesha mwanafunzi mmoja na kumpeleka kidato cha kwanza baada ya wazazi wake kumtorosha ili kumpeleka katika wilaya ya Rongido kufanya kazi hivyo watoto wasigope kutoa taarifa.



