WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema Tanzania bado ni salama kwa shughuli nza utalii pamoja na kuibuka kwa virusi vya ugonjwa wa Murbug mkoani Kagera.
Hayo yalibainishwa kwenye taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa ikiwa ni siku tano tangu Wizara ya Afya kutoa ripoti kuhusu ugonjwa huo ikieleza kuwa serikali imechukua hadhari za kutosha kudhibiti ugonjwa huo na hakuna visa vipya mpaka sasa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii, imekuwa ikiweka kipaumbele katika usalama wa wasafiri wanaowasili nchini wakati wote na pamoja na kuwa hakuna visa vipya vilivyopatikana katika maeneo ya utalii, imeendelea kuchukua hadhari.
“Tunataka kuwahakikishia wageni wanaotutembelea kwamba Tanzania imebaki kuwa mahali salama, tunafanya kila namna kuhakikisha wageni wetu wanafurahia safari zao, wakijua kwamba tunachukua hatua muhimu kulinda afya na usalama wao,” alisema Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa.
Ugonjwa huo ulithibitshwa na Wizara ya Afya kwa mara ya kwanza Machi 21, 2023 baada ya tetesi za siku kadhaa za hofu ya kuzuka kwa ugonjwa wa ajabu uliodhaniwa kuwa ni Ebola mkoani Kagera na ilielezwa kuwa ulisababisha vifo vya watu wanne kati ya watano walioambukizwa.
Machi 16, 2023, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu alithibitisha kuripotiwa kwa ugonjwa huo katika vijiji vya Bulinda na Butayaibega vilivyopo katika kata za Marua Kanyangereko wilayani Bukoba, baada ya uchunguzi ulibainika kuwa ni Murbug.