Serikali: Tumieni kiwanda cha viuadudu Kibaha

DODOMA – NAIBU Spika, Mussa Hassan Zungu ameishauri serikali kuongeza nguvu katika kutumia bidhaa ya viuadudu inayozalishwa katika kiwanda cha ndani cha Kibaha.

Alisema kwa sasa viuadudu vinavyotoka nje ya nchi dawa zina changamoto ya ubora na kuishauri serikali kuhakikisha inaongeza nguvu katika kutumia dawa hizo zinazozalishwa na kiwanda cha Kibaha.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Tweve (CCM) alitaka kujua ni halmashauri ngapi zimetekeleza agizo la Waziri Mkuu kununua dawa za viuadudu kutoka kiwanda cha Kibaha kutokomeza mazalia ya mbu.

Akijibu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk Festo Dugange alisema Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu yaliyotambuliwa katika halmashauri.

SOMA: Zeco kuilipa Tanesco kwa awamu

Alisema katika kipindi cha mwaka 2017/18 hadi 2023/24 halmashauri 146 zimenunua viuadudu lita 196,783 kwa gharama ya Sh bilioni 2.6 na kunyunyizia kwenye mazalia ya mbu.

Alisema serikali imeendelea kuzielekeza halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kununua viuadudu na kunyunyizia kwenye maeneo ya mazalia ya mbu yatakayoainishwa kote nchini.

Katika swali la nyongeza, Tweve alitaka kujua mkakati wa serikali kuongeza bajeti ili dawa viuadudu zaidi inunuliwe na kuua mazalia hatua ambayo itaokoa maisha ya wananchi.

Akijibu swali hilo, Dk Dugange alisema ofisi yake itaendelea kuongeza bajeti kwa ajili ya ununuzi wa viuadudu na kuwa katika bajeti ya mwaka 2024/25 Ofisi ya Rais-Tamisemi itabana matumizi kuhakikisha viuadudu inanunuliwa kwa wingi.

Habari Zifananazo

Back to top button