Zeco kuilipa Tanesco kwa awamu

ZANZIBAR – WIZARA ya Maji, Nishati na Madini imesema Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) hadi kufi kia Februari mwaka 2024, linadaiwa Sh bilioni tisa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na limejipanga kulipa deni hilo kwa awamu.

Waziri wa wizara hiyo, Shaibu Hassan Kaduwara aliyasema hayo jana akijibu swali la Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman aliyetaka kujua hadi sasa shirika hilo lina deni kiasi gani kutoka Tanesco na kujua mikakati kutafuta vyanzo mbadala vya nishati hiyo.

Kaduwara alisema deni hilo ni sehemu ya malimbikizo ya muda mrefu ikiwa ni matumizi ya umeme yanayofanywa na Zeco kwa wateja wake pamoja na wizara na taasisi za serikali.

Alisema shirika limejipanga kulipa deni hilo na kuitaja mikakati yake ikiwemo kuboresha miundombinu ya umeme kufunga mita zinazomtaka mteja kulipa huduma hiyo kwa kadri ya matumizi yake.

Alisema Zeco imekuwa ikifanya mawasiliano mara kwa mara na wateja wakubwa kuona hakuna malimbikizo makubwa ya madeni ikiwemo katika hoteli za kitalii.

Awali, Kaduwara alizitaja baadhi ya taasisi zinazoongoza katika madeni ya shirika hilo ikiwemo Mamlaka ya Majisafi na Salama (ZAWA) ambayo tayari serikali imeahidi kulipa kila mwezi Sh bilioni moja kwa ajili ya huduma za maji.

SOMA: Vipaumbele 3 vyajadiliwa afya ushirikiano Uingereza na serikali

Alisema Zawa ni miongoni mwa taasisi inayotumia nishati ya umeme kwa wingi kwa matumizi ya kusukuma maji katika visima vyake kwa ajili ya matumizi ya wananchi majumbani.

‘’Mheshimiwa Spika miongoni mwa taasisi za serikali zinazoongoza kwa kuwa na madeni mengi ni Zawa ambapo tunashukuru serikali imeahidi kila mwezi kulipa bilioni moja kwa ajili ya usambazaji wa huduma za maji kwa wateja majumbani,’’ alisema.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inaendelea na juhudi za kutafuta vyanzo mbadala vya nishati ya umeme na kupunguza kutegemea uzalishaji kwa asilimia 100 kutoka Tanesco.

Aliitaja kampuni ya ESL ambayo imewekeza katika uzalishaji wa umeme megawati 15 katika Kisiwa cha Pemba na kutumika katika baadhi ya visiwa vidogo ikiwemo Kokota.

Habari Zifananazo

Back to top button