Serikali ya Kasulu yaagizwa kuvutia wawekezaji

KIGOMA: MKUU wa Mkoa Kigoma, Balozi Simon Siro ameuataka Uongozi wa Serikali Wilaya ya Kasulu kuvutia wawekezaji na kuwalinda ili kutimiza lengo la serikali kuufanya Mkoa Kigoma kuwa mkoa wa kimkakati.
Balozi Siro ametoa kauli hiyo leo Julai 9, 2025 alipofanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mufindi Factory kinachoendelea kujengwa ambapo kukamilika kwake kutazalisha tani 100 za sukari kwa mwaka.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa Wilaya ya Kasulu ina maeneo makubwa na mazuri kwa ajili ya uwekezaji hasa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo hivyo lazima halmashauri na mamlaka za serikali wilayani humo zihakikishe wanavitangaza vivutio kwa ajili ya uwekezaji.

Katika ziara hiyo Balozi Siro amesema kiwanda hicho ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi ya mkoa ikiwemo kutoa ajira, kusaidia upatikanaji wa uhakika wa sukari mkoani humo lakini pia kiwanda hicho kitazalisha umeme ambao pia utatumiwa na wananchi wa Kigoma.
SOMA ZAIDI
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo, Meneja Uendeshaji wa Kiwanda hicho, Saride Satyanarayana amesema kuwa wanatarajia ujenzi wa kiwanda hicho utakaogharimu kiasi cha Sh bilioni 117 utakapokamilika mwaka 2027 ambapo sukari itaanza kuzalishwa na kwamba tayari mashamba yenye ukubwa wa hekta 30,000 yameshaanza kupandwa miwa.

Satyanarayana alisema kuwa kiwanda kitakapoanza uzalishaji kitakuwa kinazalisha sukari tani 100,000 kwa mwaka, kitazalisha karatasi za kutengeneza fedha za noti lakini pia kitazalisha umeme ambao utaweza pia kutumika na wananchi wa kawaida na kwamba ajira za watu 500 zitatolewa.



