SERIKALI ya Tanzania imeishukuru Serikali ya China kwa wazo lake la kuhamasisha wanafunzi wa Kitanzania kupenda masomo ya sayansi ili siku moja waje kuwa wana anga kama ilivyo kwa wana anga wa China.
Naibu Katibu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe alisema hayo ubalozi wa China jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya wiki ya sayansi na teknolojia China.
Profesa Mdoe alisema jana kuwa mpango huo wa China umekuja wakati mwafaka kwa kuwa kwa sasa serikali ya Tanzania iko kwenye mchakato wa kuboresha mtaala ili kuingiza mada zinazoendana na wakati huu.
“Tunafahamu umuhimu wa wahitimu wetu kuwa na ujuzi na tunajua tupo katika mapinduzi ya nne ya viwanda, hivyo lazima tuendane na mageuzi hayo na msisitizo mkubwa katika mitaala yetu utakuwa katika tehama,” alisema.
Wanafunzi kutoka Shule za William Benjamin Mkapa na Zanaki zote za Dar es Salaam walialikwa kushiriki tukio hilo la jana ubalozini hapo. Kwa kuwa wana anga watatu wa China akiwemo Chen Dong, Liu Yang (mwanamke) na Cai Xuzhe wako katika anga za juu katika kituo cha Tiangong, Profesa Mdoe alisema tukio hilo litajenga hamasa kwa wanafunzi wa Kitanzania kujikita katika masomo ya sayansi.
Wana anga hao wa China watakuwa kwenye kituo hicho cha anga za juu kwa miezi sita na kwa sasa wana miezi mitatu tangu waende anga hizo za juu. Balozi wa China hapa nchini, Chen Mingjian, alisema kituo hicho cha Tiangong kinatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuwahamasisha vijana kupenda sayansi.
Balozi Mingjian alisema mwezi Oktoba mwaka 2003, chombo cha anga za juu kinachojulikana kama Shenzhou-5 kilizinduliwa kwa mafanikio na kuwapeleka wana anga wa China kwa mara ya kwanza anga za juu. Pia alisema Juni 2012, Shenzhou-9 kikiwa kimebeba wana anga watatu kilitua katika kituo cha Tiangong-1.
Kutokana na mafanikio hayo, Mingjian alisema wanasayansi wa China wako tayari kufanya tafiti kuhusu safari za anga za juu kwa kushirikiana na wanasayansi wa Tanzania na wa nchi nyingine za Afrika.