SERIKALI imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali kama Utalii, Kilimo, Madini, Viwanda, Uvuvi na Ufugaji, kulinda viwanda vya ndani, kuvutia mitaji na uwekezaji nchini.
Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Robert Manyama amesema hayo wakati wa kupokea na kukusanya maoni unaoendelea kwa wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali kwenye Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha.
Amesema pialengo la uboreshaji huo ni kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani, kuchochea ulipaji kodi kwa hiari na kuboresha usimamizi na ukusanyaji wa kodi, ada na tozo mbalimbali.
Manyama amesema mojawapo ya maoni yaliyotolewa mwaka jana yalifanyiwa kazi ikiwemo kusamehe Kodi ya Ongezeko a Thamani(VAT) kwenye vifaa na mitambo ya kuchakata na kuhifadhi mazao ya nyuki, kusamehe VAT kwenye kwenye chai inayotengenezwa ndani ya nchi (Local Blended Tea) pamoja na Kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye madini ya dhahabu yatakayouzwa kwa viwanda vya kusafisha madini ya dhahabu nchini.
SOMA: Tume Maboresho ya Kodi yasheheni wabobezi kutimiza malengo
Amesema, Serikali pia imetoa unafuu wa kutolipa kodi ya mapato mbadala (Altenative Minimum Tax) kwenye kampuni zinazochakata mazao ya chai, kupunguza ushuru wa bidhaa kutoka shilingi 63.80 hadi shilingi 56 kwa lita ya maji ya kunywa yaliyosindikwa, kuanzisha vyanzo kwa ajili ya kugharamia Bima ya Afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalum hususan wanawake, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na kuongeza ushuru wa forodha kwenye baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Usafirishaji mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, Locken Massawe, amepongeza Serikali kwa kuonesha umuhimu wa kuwakutanisha na kusikiliza maoni yao.
“Muundo uliotumika wa kuchukua maoni unakufanya wewe mwenyewe upate imani kwamba linalokwenda mbele ya Serikali litafanyiwa kazi na serikali imelipa kipaumbele” amesistiza Massawe.
Naye Mtunza Hazina wa Jumuiya hiyo, Ester Msule, ameshukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kwa kuandaa kongamano hilo wakiwa na imani kubwa kwamba maoni yao yatafanyiwa kazi kama walivyoyawasilisha na kuwaletea mabadiliko katika biashara zao na kulipa kodi stahiki kwa manufaa ya Taifa.
“Tunashukuru Wizara ya Fedha imesikiliza kero zetu na tunajua watakwenda kuyafanyia kazi haya tuliyoyaeleza,” amesema Msule.
Aidha, Afisa Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Arusha, Sia Maruda amepongeza mpango wa kuboresha mfumo wa kodi.
“Kupitia kongamano hili tunaamini “Finance Bill” inayokuja maboresho yaliyotolewa yatawasilishwa vizuri na wafanyabiashara wameweza kupata suluhisho,” amesisitiza Marunda.