SERIKALI imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Japan huku ikitoa wito kwa kampuni za Japan kuja kuwekeza nchini katika maeneo mbalimbali katika sekta zenye maslahi ya nchi zote mbili ikiwa ni pamoja na kukuza uwekezaji binafsi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo ametoa wito huo jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Mkurugenzi Mkuu Kanda ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Naoki Yanase.
Ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kutoa wataalamu wanaofanikisha kutekeleza miradi kwa wakati na kwa viwango vya juu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya maisha ya watanzania.
Amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Japan ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya Uboreshaji wa Barabara ya Arusha-Holili, Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Maji Zanzibar Mjini na ujenzi wa barabara za mzunguko wa ndani katika jiji la Dodoma ambayo ipo katika utekelezaji.
“Tangu kuanzishwa kwa ushirikiano mwaka 1960, Tanzania imenufaika kwa kiasi kikubwa na miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Japan na hivyo kuifanya Tanzania kuwa mnufaika mkubwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara,” amesema.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya uchumi, Omolo amesema sera madhubuti za Serikali zimewezesha uchumi wa Tanzania kuendelea kuimarika ikirekodi kasi ya ukuaji wa asilimia 5.3 katika robo ya pili ya 2024, ikilinganishwa na 4.7 asilimia katika kipindi sawia cha mwaka 2023.
Aidha, mfumuko wa bei Oktoba 2024, ulifikia asilimia 3.0 ambayo ni ndani ya lengo na pia ni ndani ya wigo kwa mujibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) jambo lililochangiwa na sera nzuri za fedha, utoshelevu wa chakula na kudhibiti bei za bidhaa zinazotoka nje.
Amefafanua kuwa Septemba 2024, Kampuni ya Kimataifa inayojihusisha na kufanya tathmini ya uwezo wa nchi kuyafikia masoko ya fedha ya kimataifa ya Moody’s Investors Limited, imepandisha daraja la Tanzania kutoka B2 hadi B1.
‘’Uboreshaji hadi B1 unaonyesha rekodi ya Tanzania ya ustahimilivu wa uchumi ambayo inaruhusu Tanzania kupata kutambuliwa katika masoko ya fedha na mitaji ya kimataifa, na hivyo kuwezesha kuongezeka fursa za uwekezaji na upatikanaji mkubwa wa rasilimali fedha kwa sekta ya umma na binafsi,’’ amefafanua.
Amesema kwa sasa Tanzania inaendelea kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano, na kubainisha kuwa ana tumaini Serikali ya Japani kupitia JICA itasaidia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 ambayo inaandaliwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Afrika wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Naoki Yanase amesema Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuendeleza rasilimali watu kupitia ufadhili wa masomo.