Serikali yaja na mkakati wa kukabili utoaji mimba ‘hatarishi’

Elimu ya uzazi yasisitizwa

SERIKALI imeainisha mikakati na juhudi zinazofanywa katika kukabiliana na changamoto dhidi ya utoaji mimba usio salama.

Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel alitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike ambao wapo chini ya umri wa kuzaa.

Dk Mollel aliyasema bungeni Dodoma  wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Judith Kapinga.

Ameendelea kusema, Wizara kupitia vitengo vyake imeendelea kutoa elimu kwa klabu za vijana na vijana balehe kutojihusisha na ngono zembe ili kuepuka mimba zisizotarajiwa ambazo hupelekea kuongezeka vitendo vya utoaji mimba usio salama.

Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na utoaji mimba usio salama.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel alisema Wizara inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo ili kuwawezesha wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa.

Naibu waziri huyo alitoa wito kwa jamii kuhakikisha mimba zote zinapatikana kwa mpango ili kuondokana na changamoto ya utoaji mimba usio salama unaoweza kuathiri afya za wajawazito.

Pia, aliwataka wajawazito kuhudhuria  kliniki za uzazi wa mpango ili waweze kupatiwa elimu ya afya ya uzazi ikiwemo jinsi ya kuepukana na mimba zisizotarajiwa ili kuondokana na uavyaji wa mimba usio salama.

Habari Zifananazo

Back to top button