Serikali kuandaa wataalamu wa nyuklia

VIENNA, AUSTRIA : TANZANIA imeanza kuandaa wataalamu wa Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia kupitia vyuo vya ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujenga uwezo wa kitaifa na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema hayo Septemba 17, 2025 jijini Vienna, Austria wakati wa kikao maalum na Mkurugenzi wa Divisheni ya Afrika wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), Dkt. Gashaw Gebeyehu Wolde, kando ya Mkutano Mkuu wa 69 wa IAEA.
Katika mazungumzo yake na Theresa Wutz, Afisa Mkuu Muidhinishaji wa Miradi wa kampuni ya eee Austria, Prof. Nombo alipongeza hatua ya Austria kupitia UniCredit – Bank of Austria kuendelea kufadhili Mradi wa Elimu Kidigitali Zanzibari, akieleza kuwa msaada huo utafungua fursa za kupanua matumizi ya TEHAMA hadi shule na vyuo vya Tanzania Bara. Amesema ushirikiano huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za Serikali za kukuza ubora wa elimu kupitia teknolojia na ni mfano wa diplomasia ya uchumi inavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi.
Kukamilika kwa awamu za mradi huo kutaiwezesha Tanzania kuwa na mifumo madhubuti ya kidigitali, miundombinu imara na rasilimali watu yenye ujuzi wa kisasa katika sekta ya elimu. SOMA: Samia ataka umeme wa nyuklia