Serikali yakanusha kuuza bandari ya Bagamoyo

DAR ES SALAAM – Serikali ya Tanzania imekanusha uvumi unaodai kuwa mamlaka zake zimeuza Bandari ya Bagamoyo kwa Kampuni ya Uwekezaji na Maendeleo ya Saudi Arabia (SADC).
Uvumi huo ulienea baada ya kusambaa kwa picha katika mitandao ya kijamii zikimuonesha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, akiwa pamoja na ujumbe wa wawekezaji kutoka Saudi Arabia na viongozi wa serikali. Baadhi ya taarifa zilidai kuwa picha hizo zilikuwa sehemu ya makabidhiano rasmi ya bandari hiyo.
Aidha, Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA) lilimnukuu Mwenyekiti wa Shirikisho la Chemba ya Wafanyabiashara wa Saudi Arabia, Hassan Al-Huwaizi, akidai kuwa Tanzania imeipa SADC haki za umiliki na uendeshaji wa Bandari ya Bagamoyo.
Soma zaidi: EPZA yazungumzia ujenzi zaidi viwanda Bagamoyo
Hata hivyo, afisa mwandamizi wa serikali, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amekanusha madai hayo akisema:
“Taarifa hiyo haina ukweli. Ni kweli kwamba viongozi wa Bandari ya Tanzania na baadhi ya Mawaziri walihudhuria mkutano na wawekezaji kutoka Saudi Arabia, lakini kilichojadiliwa ni mpango wa kibiashara wa pamoja, si uhamishaji wa umiliki wa bandari.”
Afisa huyo alifafanua kuwa makubaliano yaliyofanyika yalikuwa ya ishara tu, na hakuna mkataba wowote rasmi uliosainiwa kuhusu umiliki wa bandari hiyo.
“Tunapenda kuufahamisha umma kuwa picha zilizosambaa zilihusiana na majadiliano ya uwekezaji, si makabidhiano rasmi. Kutakuwa na hafla rasmi ya utiaji saini endapo pande zote mbili zitakubaliana kwa mujibu wa taratibu za kisheria,” aliongeza.
Soma zaidi: TPA yaiwekea mikakati Bandari ya Bagamoyo
Mpango wa uwekezaji wa Saudi Arabia katika Bandari ya Bagamoyo ni sehemu ya mradi wa East Gateway Project, unaolenga kuimarisha nafasi ya Saudi Arabia kama kitovu cha biashara duniani na kuongeza uwekezaji wake barani Afrika.
Katika Jukwaa la Biashara kati ya Saudi Arabia na Tanzania, lililoandaliwa kwa usaidizi wa Chemba ya Biashara ya Saudi, viongozi wa pande zote mbili walijadili fursa mpya za uwekezaji, ikiwemo miradi ya maendeleo Zanzibar, kama sehemu ya mkakati wa Saudi Arabia kupanua uwepo wake katika masoko ya Afrika.
Mpaka sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wala Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, Mipango na Uwekezaji kuhusu suala hilo.



