Serikali yapendekeza bajeti tril 62/-, vipaumbele vitano

SERIKALI imetaja vipaumbele vitano katika mapendekezo ya mfumo na ukomo wa bajeti kwa mwaka 2026/2027.

 

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alisema hayo wakati wa kuwasilisha mapendekezo ya Mfumo na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/2026 katika mkutano wa wabunge wote Dodoma jana.

 

Balozi Omar alisema serikali inakadiria kukusanya na kutumia Sh trilioni 62.33 kwa mwaka 2026/2027 sawa na ongezeko la asilimia 10.3, ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/2026 ya Sh trilioni 56.49.

 

Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni utawala, amani, usalama na utulivu, kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani utakaotekelezwa kupitia sekta tisa za mageuzi.

 

Pia, alieleza vipaumbele vingine ni kujenga uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na vichocheo vya mageuzi.

 

Alisema serikali itaweka msukumo katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, ulipaji wa mishahara na deni la serikali, ukamilishaji wa miradi na programu za maendeleo zinazoendelea na kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia ushiriki wa sekta binafsi, kuwekeza katika miradi yenye tija itakayochochea ukuaji wa uchumi, kuongeza fursa za ajira na mapato kwa serikali.

 

Mapato

 

Aidha, Balozi Omar alisema kwa kuzingatia sera za bajeti na mikakati ya kukusanya mapato na udhibiti wa matumizi, serikali inakadiria kukusanya na kutumia Sh trilioni 62.33.

 

Alisema ukomo unazingatia vigezo vya mwenendo halisi wa mapato ya ndani, ukomo wa nakisi ya bajeti usiozidi asilimia tatu ya Pato la Taifa, ongezeko la deni la serikali, gharama za mikopo katika soko la fedha na ongezeko la malipo ya mikopo, mahitaji ya ajira mpya na mabadiliko ya sera za washirika wa maendeleo.

 

Balozi Omar alisema mapato yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 46.79, mapato ya kodi yakiwa ni Sh trilioni 36.99 huku mapato mengine ni Sh trilioni 9.24, ikiwamo mapato ya mamlaka za serikali za mitaa ya Sh trilioni 1.97 na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo Sh bilioni 563.1, wakati makadirio ya mapato ya ndani (kodi na mengine) ni sawa na asilimia 74.2 ya bajeti ya mwaka 2026/2027.

 

“Kwa kuzingatia malengo ya Dira 2050, serikali itaendelea kutumia njia mbadala za kugharimia miradi na kuandaa miradi inayokopesheka ili sekta binafsi itumie fursa hiyo kuwekeza katika miradi ya maendeleo.”

 

Matumizi

 

Balozi Omar alisema serikali imepanga matumizi na uwekezaji katika mali zisizo za kifedha, bila kujumuisha malipo ya mtaji ni Sh trilioni 54.5 ambapo kati ya kiasi hicho stahiki za watumishi ikijumuisha michango ya pensheni ni Sh trilioni 9.99, gharama za bidhaa na huduma Sh trilioni 8.3, malipo ya riba Sh trilioni 7.26, ruzuku Sh trilioni 24.94 na uwekezaji katika mali zisizo za kifedha Sh trilioni tatu.

 

Alisema serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 15.54 na kati ya kiasi hicho, mikopo ya ndani ni Sh trilioni 6.56, mikopo ya nje yenye masharti nafuu Sh trilioni 6.56 na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara Sh trilioni 2.43, wakati mikopo halisi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Sh trilioni 7.71 na malipo ya mtaji ni Sh trilioni 7.84.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button