Serikali yapewa mbinu kuilinda Shilingi
DAR ES SALAAM – WATAALAMU na wachambuzi wa masuala ya uchumi wameshauri yafanyike mambo matano kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Mambo waliyotaja ni pamoja na kuongeza uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa ili kuuza nje na kuongeza hifadhi ya dhahabu Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mengine ni uwekezaji katika viwanda kupunguza kuagiza bidhaa nje, kuhamasisha matumizi ya gesi asilia na kutumia Shilingi hata kwa hoteli za ndani kwamba yakizingatiwa itawezesha kuongeza thamani ya sarafu hii ya Tanzania.
Dola ya Marekani jana ilinunuliwa kwa Shilingi 2,718 za Tanzania. Mchambuzi wa masuala ya uchumi na fedha, Profesa Haji Semboja alisema Tanzania ina dhahabu ya kutosha lakini haijatumika kuongeza thamani ya Shilingi.
Profesa Semboja alisema mwaka 2017 ilitungwa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali namba 5 ya mwaka 2017 iliyolenga kufanya rasilimali ziweze kunufaisha Watanzania.
Alilieleza HabariLEO kuwa sheria hiyo ilitangaza mamlaka ya kudumu ya Watanzania kuhusu mali na maliasili zote na inaeleza kuhusu unyonyaji wa rasilimali kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.
“Jambo la msingi ni Watanzania kumiliki na kuziendeleza rasilimali zote ikiwemo madini na gesi kufuatana na sheria kwa kufanya hivyo, nchi hiyo tajiri haipaswi kupata changamoto kama hizo endapo itatumia rasilimali zake kuzalisha na kuuza,” alisema Profesa Semboja.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Walter Nguma alisema wanapima kushuka kwa Shilingi kwanza kwa kuangalia uwezo wa fedha hiyo kwenye masoko duniani kama inakuwepo na uwezo wake kwenye ununuzi.
Nguma alisema wanalinganisha thamani ya sarafu hiyo na fedha nyingine ambazo zina nguvu kwenye masoko duniani ikiwemo Dola ya Marekani au Pauni ya Uingereza.
Alisema fedha ya Tanzania imekuwa ikishuka thamani ikimaanisha kuwa inakosa nguvu kwenye soko la kibiashara ikilinganishwa na fedha nyingine. Alisema kushuka thamani ya Shilingi ni mkakati wa nchi nyingine kuidhoofisha na kuimarisha fedha zao hivyo kupata faida.
SOMA: ‘Hatua zinachukuliwa kulinda thamani ya shilingi’
Nguma alipendekeza kuhamasisha uwekezaji kwa kujenga viwanda vya bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa kwa wingi kupunguza kuagiza bidhaa nje ya nchi. Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Dk Godvictor Lyimo alisema kushuka au kupanda kwa thamani ya Shilingi kunatokana na mizania ya nchi inavyouza nje na inavyonunua.
Alisema sababu ya kushuka kwa thamani ya Shilingi mara kwa mara inatokana na kuwepo kwa miradi mikubwa inayotumia fedha za kigeni kuagiza vifaa mbalimbali.
“Tujitahidi kuongeza mauzo yetu yaliyoongezewa thamani kwenye masoko ya nje ili kuleta fedha nyingi za kigeni. Tujikite kwenye uzalishaji,” alisema Dk Lyimo.
Alisema sekta ya kigeni pia inapaswa kuongezewa uwekezaji na kutangaza vivutio vya kitalii vilivyopo nchini kwani inachangia upatikanaji wa fedha za kigeni.
“Matumizi ya nishati ya mafuta inachangia kwa kiasi kikubwa kutumia fedha za kigeni, tuweke nguvu katika gesi asilia ambayo tumejaliwa na Mungu hii itapunguzia matumizi ya fedha kuagiziwa mafuta,” alisema Dk Lyimo.
Dk Lyimo alisema hifadhi kwa njia ya dhahabu ni njia mojawapo ya kulinda thamani ya Shilingi kwani Tanzania kuna dhahabu nyingi.