Serikali yapokea maoni zaidi kuhusu tozo

SERIKALI imesema inaendelea kupokea ushauri na maoni kuhusu tozo baada ya uamuzi wa kufuta na kupunguza baadhi uliotolewa bungeni juzi.

Imesema uamuzi uliotolewa juzi na Wizara ya Fedha na Mipango ya kufuta tozo tatu za miamala ya kielektroniki kuanzia Oktoba Mosi, mwaka huu na kupunguza gharama ya miamala, sio mwisho bali inaweza kufanya marekebisho pindi ikionekana yafaa.

Pia imesema inaendelea na mikakati ya kupanua wigo wa walipa kodi kwa kuhakikisha wote wenye sifa za kulipa kodi wanafanya hivyo ili kuongeza vyanzo vya mapato ili serikali itekeleze mipango ya maendeleo kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa Jumatano Dar es Salaam na Kamishna Msaidizi wa Uchambuzi wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, William Mhoja alipozungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini kuhusu hatua ya serikali ya kufuta tozo za miamala ya kielektroniki.

Mhoja alisema serikali ni sikivu na hatua iliyochukua na kutangazwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ya kufuta tozo tatu za miamala ya kielektroniki, ni ya kupunguza gharama kwa wananchi na kuwa maoni zaidi na ushauri yanaendelea kupokelewa.

“Kwa sasa hatua zilizochukuliwa na serikali ni hizo za kufuta tozo na kupunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi 50 kulingana na kundi la muamala husika, bado serikali inaendelea kupokea ushauri na maoni kuhusu tozo,” alisema Mhoja.

Aliongeza: “Ila kwa sasa hatua zilizochukuliwa ni hizo na kinachofanywa kuanza utekelezaji wake ni kuandaa kanuni ili Oktoba Mosi utekelezaji ukianza kanuni ziwepo.”

Alisema uamuzi huo wa serikali wa kufuta tozo hizo umewashirikisha pia wadau mbalimbali wakiwamo benki, wananchi na wengine na kwamba yapo pia maoni ya wananchi wanaotaka tozo zote zifutwe na kuwa huo ni ushauri umepokelewa na serikali itaifanyia kazi.

Akizungumzia mikakati ya serikali katika kupanua wigo wa walipakodi nchini, Mhoja alisema kampeni ya dai risiti, toa risiti ni moja ya mkakati wa serikali kuhakikisha kila malipo yanapofanywa kodi ya serikali inalipwa.

“Niwaombe wananchi wote, kila mnapofanya manunuzi dai risiti, usipodai muuzaji halipi kodi ya serikali, ila ukidai risiti kodi inalipwa na ndiyo inatumika kutekeleza miradi ya maendeleo yetu, tuache tabia ya kushirikiana na wauzaji ambao wanauza bila risiti,” alisema Mhoja.

Aliitaja hatua nyingine ya kuongeza wigo wa walipakodi ni kuhakikisha wananchi wote wanaostahili kulipa kodi wanalipa na hiyo ni pamoja na kuwaingiza kwenye mfumo wa walipakodi walipakodi wapya.

Juzi bungeni Dodoma, Dk Mwigulu alitoa kauli ya serikali ikionesha imefuta tozo tatu za miamala ya kielektroniki kuanzia Oktoba Mosi, mwaka huu.

Dk Mwigulu alitaja tozo hizo ni kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote), kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote) na tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine (pande zote).

Aidha, serikali imesamehe tozo ya miamala ya kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na mashine za kutolea fedha (ATM) kwa miamala yenye thamani isiyozidi Sh 30,000.

Pia imepunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi 50 kufuatana na kundi la miamala, na kwamba baada ya kanuni kukamilika punguzo hilo litaeleweka kwa kila kundi.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button