WADAU wa masuala ya diplomasia na uchumi wameipongeza serikali kuanzisha hadhi maalumu kwa ajili ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) na sasa wamechukua uraia wa mataifa mengine.
Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ililieleza Bunge kuwa itawapa hadhi maalumu Watanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine ili wachangie maendeleo ya nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema Watanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine na kuukana utanzania watapewa fursa zaidi ya 10 nchini baada ya serikali kuona umuhimu wao kuchangia maendeleo hasa ya kiuchumi.
Masauni aliwaeleza wabunge kuwa hadhi na fursa hizo kwa Watanzania zitatekelezwa baada ya taratibu za serikali kukamilika yakiwemo marekebisho ya sheria.
Uraia wa Tanzania unaongozwa na Sheria ya Uraia ya Tanzania Sura ya 357 rejeo la mwaka 2002.
“Sheria hii inabainisha aina tatu za uraia wa Tanzania ambazo ni uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi na uraia wa tajnisi.
“Kwa mujibu wa Sheria ya uraia hiyo serikali hairuhusu uraia pacha kwa watu wazima isipokuwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 ambao wanakuwa na uraia wa Tanzania na uraia wa nchi nyingine”.
Mchambuzi wa masuala ya siplomasia na siasa, Goodluck Ng’ingo alisema uamuzi wa serikali kutoa hadhi maalumu kwa diaspora ni muhimu kwa nchi na Watanzania.
“Ukitazama Katiba yetu haijazungumzia suala la uraia pacha bali imetoa sifa za kuwa Mtanzania na sifa ya mgombea wa nafasi ya urais.
“Changamoto ya uraia pacha ni je mwenye uraia pacha akiwa nje ya mipaka ya nchi anawajibishwa kwa sheria ipi?
“Kwa sababu kuna mambo ni haki kwa uraia wa taifa moja alilonalo, lakini sio haki kwa Tanzania, je mtu huyo unamuwajibishaje na kwa sheria gan?” alihoji Ng’ingo.
Alisema bado suala la uraia pacha kwa Tanzania si la kukubalika kwa sasa kwa mustakabali wa usalama na ulinzi wa nchi na hatua ya serikali kuja na hadhi maalum ndio tamanio la wengi linalotoa fursa ya diaspora kunufaika na asili yao.
Diaspora mwenye asili ya Tanzania aishiye Marekani na ambaye sasa ni raia wa taifa hilo, Ernest Makuliro alisema uamuzi wa Serikali ya Tanzania kutoa hadhi maalumu utatoa fursa nyingi kwao.
“Hili ni jambo jema, litasaidia diaspora walio nje kunufaika na fursa nchini Tanzania na kuwapunguzia gharama za tozo na malipo mengine pindi waingiapo nchini, hata mimi sasa pamoja kuwa nimeukana Utanzania na kuwa raia wa Marekani nimefurahi nitaanza kuwekeza kwenye nchi ya asili yangu, awali sikuweza kwa kukosa sifa,” alisema Makuliro.
Mchambuzi wa masuala ya diplomasia, siasa na uchumi, Henry Mwang’onda alisema diaspora wengi wanatamani kupata hadhi za asili ya mataifa yao hivyo kuwapa hadhi kutawawezesha kuzitumia fursa nchini zikiwamo za kuwekeza.
Mwan’onda alipinga suala la kuwa na uraia pacha akidai kuwa utawapa hadhi sawa na raia wengine waishio nchini hata kuwania nafasi ya kugombea urais wa nchi jambo alilodai ni hatari kwa usalama wa nchi.
Masauni aliwaeleza wabunge kuwa serikali bado haijajiridhisha kama uraia pacha ni takwa la wananchi wengi.