SERIKALI imesema imefanya jitihada kubwa ya kupunguza changamoto za biashara nchini hususani kupunguza utitiri wa tozo kutoka 380 hadi 148 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2020/2021.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande ameyasema hayo bungeni Dodoma leo Juni 28, 2023 akijibu swali la msingi la Mbunge wa Buhigwe, Kavejuru Felix (CCM).
Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuondoa changamoto za biashara za mpakani hasa utitiri wa tozo.
Akijibu swali hilo, Chande amesema utozwaji wa kodi ya forodha kwa bidhaa zinazoingia nchini kutoka nje ya jumuiya ya Afrika ya Mashariki unasimamiwa na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya Mwaka 2004.
Amesema kodi zinazotozwa kwa bidhaa zinazoingia nchini ni pamoja na ushuru wa forodha ambayo ni ya Afrika Mashariki, kodi ya VAT ambayo hutozwa na kila nchi mwanachama, kodi ya ushuru wa bidhaa ambayo hutozwa kwa baadhi ya bidhaa na tozo ya maendeleo ya reli.
Aidha, amesema tozo nyingine hutozwa kwa huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za serikali zinazohusika na uondoshwaji wa mizigo mipakani, ambazo husimamiwa kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha taasisi hizo.
Chande amesema, serikali itaendelea kuondoa changamoto za kufanya biashara nchini ikiwemo sehemu za mipakani.
Comments are closed.