Serikali yasaini mkataba ujenzi kituo cha moyo

SERIKALI ya Tanzania na China leo zimesaini mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kupanua Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) kwa kujenga kituo cha moyo eneo la Mloganzila jijini Dar es Salaam.

Upembuzi huo utakaochukua muda wa miezi mitatu utaruhusu ujenzi wa kituo hicho kuanzia mwaka ujao, ambapo utakamilishwa ndani ya miaka miwili.

Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof Tumaini Nagu, amesema lengo ni kufanya JKCI kuwa kituo bora cha matibabu ya moyo Afrika.

“Leo tumesaini mkataba ni wakati ambao sisi wote tulikuwa tunasubiri kupanua taasisi hii kwa niaba ya serikali, naishukuru China kwa kuendelea kudumisha uhusiano mzuri na tumekubaliana kati ya serikali mbili kuanza kufanya upembuzi yakinifu ya kuboresha JKCI, ili  ikue zaidi,”ameeleza Prof Nagu.

Amesema serikali ya China imefanya mambo mengi kama kujenga miundombinu na majengo mbalimbali ikiwemo jengo la sasa la JKCI, imechangia kwa asilimia kubwa kufanikisha.

Amebainisha kuwa kwa sasa JKCI wamekuwa wakitoa huduma ya moyo Afrika mashariki na Kati, hivyo huduma inahitajika kwa wingi kwa sababu wagonjwa wanaongezeka.

“Waziri wa Afya alitembelea China 2018 na aliwaomba tuweze kutanua wigo wa JKCI na kuongeza ufanisi ili kiwe kituo cha umahiri na Serikali ya China imeridhia na wametuma wataalamu kuangalia na leo tumesaini,  ambapo sasa tunaruhusu upembuzi yakinifu tuone uwezekano wa kujenga kituo,”amefafanua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema kwa siku moja wanaona wagonjwa 400 wa nje huku waliolazwa wakiwa ni 100.

Amesema kutokana na wagonjwa kuongezeka jengo hilo limekuwa dogo, hivyo serikali imeona iongeze lingine ili kukidhi mahitaji.

Habari Zifananazo

Back to top button