Serikali yasitisha zoezi la utambuzi mifugo

Ni takribani mifugo milioni 5 tu kati ya milioni 45 ambayo imefikiwa na zoezi hilo

SERIKALI imesitisha zoezi la kufanya utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kieletroniki kipindi cha miezi mitatu kwa lengo la kufanya tathmini.

Akitoa taarifa Bungeni Dodoma leo asubuhi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa hadi sasa ni mifugo milioni tano iliyofikiwa na huduma hiyo kati milioni 45, jambo linalodhihirisha kuwa zoezi hili linakabiliwa na changamoto.

Sheria ya kufanya utambuzi wa mifugo ilipitishwa mwaka 2010 na kanuni zake zilitungwa 2021.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema serikali imechukua hatua kadhaa kuboresha sekta ya mifugo kwa kuondoa tozo kadhaa na kutoa ruzuku.

“Serikali imeendelea kutafuta soko la nyama nje ya nchi….tunaendelea kuwasihi wafugaji wafuge kisasa,” amesema Waziri Mkuu.

Baada ya kuwasilisha ripoti hiyo, Mbunge Aida Kenan alihoji ikiwa kuna mpango wa kurejesha malipo yaliyokwishafanyika kwa ajili ya zoezi hilo.

Kuhusu hilo, Waziri Mkuu amesema zoezi hilo limesitishwa kwa muda hadi Januari, 2023 ili kubaini changamoto zilizojitokeza huku akiongeza kuwa suala la bei litaamuliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gharama ya kuweka hereni kwa ng’ombe mmoja na 1,750/- huku mbuzi na punda ikiwa ni 1,000/- kila mmoja.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button