S ERIKALI imesema inachukua hatua za muda mfupi na muda mrefu kudhibiti kupanda bei ya bidhaa za chakula kama vile mchele, mahindi na maharage.
Katika uchunguzi uliofanywa na HabariLEO katika masoko takribani manne mkoani Dar es Salaam, bei za vyakula zinazidi kuongezeka na sasa mchele na maharage vimefikia bei ya juu Sh 4,000 kwa kilo kutoka ya awali ilikuwa Sh 1,900 hadi 2,000.
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Axaud Kigahe alisema jana kwa njia ya simu kuwa mkakati wa serikali wa muda mfupi ni kutoa taarifa sahihi wapi kunapatikana bidhaa gani na kwa shilingi ngapi ili mtu anayenunua anunue kwa bei sahihi.
Kigahe alisema katika mkakati wa muda mrefu, serikali inaweka fedha za kutosha za ruzuku ya mbolea na kuhakikisha miundombinu ya kusafirisha inaboreshwa na zaidi imeongezeka bajeti kwenye kilimo kutoka Sh bilioni 200 mpaka bilioni 900.
“Sasa zaidi ya shilingi bilioni 700 zimewekwa kwenye kilimo ili hata ikitokea mvua hakuna kilimo cha umwagiliaji kiendelee,” alisema Kigahe.
Alisema wizara yao imeingilia kati suala hilo kwa kuona na kupata taarifa sahihi za bei za bidhaa hususani kutoka kwa wakulima ili kujua wanauza shilingi ngapi na kwenye masoko pia zinauzwa shilingi ngapi.
Alisema bidhaa zikiwa nyingi sokoni na wanunuzi wakiwa wachache maana yake bei zitashuka, lakini bidhaa zikiwa chache maana yake wanunuzi wengi bei zitapanda na kusisitiza kuwa hiyo ndio hali halisi ya sasa.
“Lakini nadhani hii sasa ni fursa kwa wakulima ya kulima zaidi kwa sababu sasa hivi vijijini gunia la mahindi la debe saba wanauza shilingi 140,000 mpaka 150,000 maana yake mkulima naye anaanza kupata faida ya kilimo chake,” alisema Kigahe.
Alisema zamani wakulima waliuza hadi magunia matano kununua mfuko mmoja wa mbolea jambo ambalo halikuwa sahihi na liliwaumiza, lakini sasa angalau wana uhakika wa kuuza gunia moja na kununua mbolea na kupata mazao mengi na kufikia hatua ya kupunguza bei kutoka Sh 120,000 ya sasa hadi Sh 70,000.
Alieleza kuwa bei za vyakula hazijaanza kupanda kipindi hiki cha Novemba, ila zilianza mapema kutokana na sababu nyingi ikiwemo vita ya Ukraine na Urusi kwa upande wa ngano na unga na baadaye changamoto ya kilimo kutokana na hali ya hewa mvua mwaka jana zilikuwa chache na kusababisha mavuno kutokuwa mazuri sana maeneo yote kuanzia mpunga na mahindi.
Alitaja sababu nyingine ya bei hizo ni changamoto za mafuta kwa maana ya usafirishaji gharama kutoka sehemu moja kwenda nyingine na ndio maana serikali inajitahidi kutatua changamoto hiyo kupitia ruzuku ya mafuta.
“Kwa sasa hivi nitoe mwito kwa wafanyabiashara wanaopenda kuongeza bei kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na sikukuu, si vizuri tuna taarifa sahihi za bei kutoka kwa wakulima, tunaamini bei zitakazowekwa si zile za kumuumiza mlaji,” alisema Kigahe.
Aliongeza: “Tutashirikiana na wenzetu wa Tume ya Ushindani tuone bei hii imeongezeka kiasi gani ili kuona namna ya kudhibiti wasizidishe zaidi ya kile kiwango ambacho ni sahihi kulingana na bei za kutoka kwa wakulima.” Kuhusu mazao kuuzwa nje, alisema moja ya lalamiko kubwa la wakulima ilikuwa kwa nini masoko ya nje yanafungwa pale wanapotaka kuuza, wakidai wanapolima hawapangiwi lakini wanapotaka kuuza wanapangiwa.
“Sasa tukaona si sahihi, serikali ilichofanya ni kuhakikisha kunakuwa na akiba ya kutosha ya chakula halafu baada ya hapo tunaruhusu mtu auze kwa soko analoona yeye ikiwemo masoko ya nje lakini tunatoa tahadhari mwananchi anapouza ahakikishe na yeye amejiwekea akiba asiuze chakula chote,” alisema Kigahe.
Meneja wa Soko la Machinga Complex, Dar es Salaam, Stella Mgumia alikiri kuwa hali ya bidhaa katika soko lake si nzuri kutokana na kuendelea kupanda siku hadi siku na sasa mchele unauzwa kuanzia Sh 2,700 hadi 3,800 wakati maharage bei ya chini ni Sh 3,900.
Aidha, katika Soko la Gongolamboto, mchele unauzwa kuanzia Sh 3,200 hadi 3,800, masoko ya Mwananyamala, Manzese, Shekilango na Magomeni bei ya mchele ya chini ni Sh 2,700 na ya juu kabisa ni Sh 3,600, maharage bei ya chini ni Sh 3,900 kwa kilo.