Serikali yatangaza ajira sekta ya afya, elimu

Yatadharisha kuepuka matapeli

SERIKALI imetangaza ajira 21,200 kwa kada ya walimu na afya huku ikitahadharisha waombaji wa ajira hizo kupeuka matapeli watakaowapigia simu na kuwataka kutoa fedha kwa ajili ya kupata ajira kwa kuwa ajira hizo ni bure.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa Angellah Kairuki akizungumza leo Aprili 12, 2023 amesema vigezo na masharti vitatumika katika kuwaajiri watumishi hao na si vinginevyo.

“Natoa rai kwa waombaji, mtu asije akapigiwa simu kuombwa fedha kwa ajili ya kupata ajira hizi, msiingie katika huo mtego kwa kuwa ikibainika  hilo limejitokeza  toeni taarifa kwa mamlaka ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya matapeli.” Amesema Kairuki.

Amesema, idadi ya watakaoajiriwa katika kada za Ualimu ni 13,130 ambao watafundisha katika  shule za msingi na Sekondari na kada ya afya 8,070 watakaofanya kazi katika Hospitali za Wilaya, Vituo vya afya na Zahanati

Kairuki amesema  mchakato wa kuajiri  watumishi hao umeanza leo  Aprili 12 ,2023 hadi  Aprili 25, 2023 ambapo waombaji wa nafasi za ajira katika kada ya ualimu na afya  wanatakiwa  kuwa wamehitimu  kwenye vyuo  vya elimu ya juu na kati kwenye fani ya ualimu na afya vinavyotambuliwa na Serikali.

Ameendelea kufafanua kuwa nafasi zilizopo ni kwa wahitimu wa Astashahada (Certificate),  stashahada (Diploma) na shahada (Degree) ambapo sifa za kitaaluma zimeanishwa kwa waombaji wa kada za ualimu wa shule za msingi na sekondari pamoja na fani mbalimbali za kada ya afya kama zilivyoainishwa katika tangazo la ajira  na katibu Mkuu Ofisi ya Rais –TAMISEMI

Amesema waombaji  wa kada ya ualimu wawe wamehitimu kuanzia mwaka 2015 hadi 2022 na kwa kada ya afya wasizidi umri wa miaka 45, hivyo amewataka waombaji hao kuanza kutuma  maombi  yao kuanzia leo  Aprili 12, 2023 hadi   25 Aprili 25, 2023 saa 5:59 usiku.

Waziri Kairuki amewataka waombaji waliowahi kutuma maombi ya ajira kupitia mfumo wa maombi ya ajira  kuhuisha taarifa zao  kwenye  mfumo wa ajira kupitia kiunganishi ajira.tamisemi.go.tz kwa kutumia namba ya mtihani wa kidato cha nne na nywila au kuomba upya .

Aidha, amewataka waombaji wa ajira hizo kuwa tayari kufanyakazi kwenye Halmashauri na vituo watakavyopangiwa, kufanyakazi na mashirika au taasisi zilizoingia ubia na Serikali na baada ya kupangiwa kituo cha kazi hakutakuwa na nafasi ya kubadilishiwa kituo cha kazi

Habari Zifananazo

Back to top button