Serikali yatangaza hatua kudhibiti ebola

WIZARA ya Afya imetangaza hatua mpya za kuzuia kuingia na kusambaa kwa virusi vya ebola.

Kumekuwa na taarifa za kuwapo kwa ugonjwa wa ebola katika nchi jirani ya Uganda na Septemba 19, mwaka huu, kiliripotiwa kifo cha mtu mmoja kutokana na ugonjwa huo.

Baada ya kifo hicho, Septemba 22, mwaka huu Uganda iliripoti kuwapo kwa wagonjwa sita wa ebola waliothibitishwa na kuongeza idadi ya maambukizi hadi saba.

Licha ya Wizara ya Afya nchini hapa kutangaza kuwa hakuna kesi iliyosajiliwa nchini, serikali imetoa mwito kwa raia kuzingatia hatua za kuzuia maambukizi.

Waziri wa Afya, Daniel Ngamije, alisema Serikali inafanya kazi kwa karibu na ushirikiano na wenzao wa Uganda.

“Tunashirikiana kwa karibu na taasisi nyingine kufuatilia kuenea kwa ugonjwa huo katika nchi jirani hasa Uganda ambako kisa cha ugonjwa wa ebola kilithibitishwa katika Wilaya ya Mubende. Wizara zote za afya nchini Rwanda na Uganda zinafanya kazi pamoja ili kuimarisha hatua za kuzuia katika mipaka ya nchi kavu, uwanja wa ndege na ndani pia,” alisema Ngamije.

Ugonjwa wa ebola huambukizwa kupitia majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa.

Dalili za ebola ni pamoja na homa, maumivu ya viungo, maumivu ya kichwa, koo, uchovu, kuhara, kutapika, upele wa ngozi, macho mekundu, maumivu ya tumbo na kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili.

Wizara ya Afya inasisitiza: “Epuka kugusa damu na majimaji ya mwili, vitu ambavyo vinaweza kuwa vimegusana na damu au majimaji ya mtu aliyeambukizwa, epuka kugusa mwili wa mwathirika wa ebola au mnyamapori aliyekufa au kula nyama yake. Nawa mikono kila mara kwa sabuni na maji safi na utafute matibabu unapojisikia vibaya.”

 

Habari Zifananazo

Back to top button