Serikali yatathmini usafirishaji data kupunguza makali

SERIKALI inafanya tathmini ya usafirishaji wa data hatua ambayo inaweza kupunguza gharama za usafirishaji wa data hivyo kupungua gharama za vifurushi kwenye mitandao ya simu.

Pia imepanga kupitia upya kanuni zinazosimamia watoa huduma na wanaotumia huduma za mawasiliano na kuyafanyia kazi mapungufu yatakayobainika. Haya yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati wa kuchangia Mapendekezo ya Mwongozo wa maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2023/2024, Bunge zima lilipokaa kama kamati ya mpango.

Amesema kila baada ya miaka mitano, serikali imekuwa ikifanya tathmini ya gharama za kusafirisha data na kuwa tathmini ya mwisho ilifanyika mwaka 2018 na kutoa tathmini ya wastani wa Sh mbili mpaka Sh tisa.

“Kwa sasa tumeanza tathmini hiyo na ifikapo Desemba mwaka huu itakamilika na kuwa na mwelekeo kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanyika na taratibu za kikodi zinazochukuliwa tunadhani matokeo ya tathmini ni gharama za usafirishaji wa data kushuka,” alisema. Kuhusu kanuni, Nape alisema, “hatufurahishwi na mahusiano kati ya watoa huduma za mawasiliano na watumiaji wa huduma za mawasiliano hakuna mahusiano mazuri kumekuwa na mashaka makubwa na kutuhumiana sana.”

Alisema kutokana na hali hiyo, serikali inapitia kanuni hizo hususani kwenye wajibu wa mtoa huduma na mtumiaji huduma za mawasiliano. “Tunadhani kuna mapungufu ya kanuni zinazosimamia watoa huduma na watumiaji huduma za mawasiliano katika kuzipata hizi huduma na hasa kwenye maeneo ya wajibu wa watoa huduma na wajibu wa watumishi huduma.

“Serikali tumefanya uamuzi wa kuzipitia upya kanuni hizi ili tuone mashimo yako wapi ili mahusiano haya yarekebishwe ili huduma za mawasiliano nchini ziboreshwe na hasa mawazo ya wabunge na wananchi,” alisema. Aidha, Nape alisema serikali imemuagiza mtoa huduma kuwalipa MB 200 alizowakata kizembe wateja walionunua vifurushi kwa kutumia bango lililokuwa halijabadilishwa taarifa za bei.

Nape bila kumtaja mtoa huduma, alisema mtoa huduma aliyelalamikiwa kuwauzia vifurushi wateja visivyolingana na bango la bei ya vifurushi vyao, amekiri kufanya hivyo. Alisema wateja wa kampuni hiyo 22,107 walioathirika kwa kutumia huduma ya mtoa huduma huyo kabla ya taarifa za bei ya vifurushi hazijabadilika.

“Baada ya kung’amua hili serikali imemuagiza mtoa huduma kwanza awarudishie walioathirika MB zao 200 walizotakiwa kupata kulingana na bango lake aliloliweka,” alisema.

Alisema pia awape MB 300 kila mtu aliyeathirika kama fidia ya usumbufu alioupata kwa sababu ya uzembe uliofanywa na mtoa huduma. Nape alisema wamemtaka mtoa huduma awaombe radhi watumiaji wa huduma hiyo walioathirika kwa kuwatumia ujumbe kwenye simu zao kueleza uzembe alioufanya.

Kuhusu wateja wa simbaking kulazimishwa kuwa na salio wakati wanapotaka kufanya miamala ya kifedha kutoka benki, Nape alisema makampuni mengi yameweka fursa ya kukopeshwa salio wakati ambapo huna salio katika simu.

Habari Zifananazo

Back to top button