Serikali yatumia Sh bil 17 waathirika mabomu Mbagala

Serikali yatumia Sh bil 17 waathirika mabomu Mbagala

SERIKALI imelipa kiasi cha Shilingi bilioni 17.46 kwa waathirika wa mlipuko mabomu yaliyotokea katika Kambi ya JWTZ Mbagala, Dar es Salaam Aprili 29, 2009.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, amesema kiasi hicho kilicholipwa kwa wananchi 12,647 si fidia bali ni mkono wa pole kwa walioathiriwa na janga hilo.

Amelazimika kutoa maelezo hayo leo bungeni, jijini Dodoma leo, Jumatano, Oktoba 2, 2022, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbagala, Abdalah Chaurembo, aliyetaka kufahamu kauli ya serikali juu ya mapunjo ya fidia kwa wananchi walioathirika na mlipuko wa mabomu jimboni kwake.

Advertisement

Akieleza zaidi, Simbachawene amesema, malipo hayo, yalitolewa kwa awamu sita kuanzia mwaka 2009 hadi 2020.

“Vile vile, Serikali ilitoa kifuta machozi pamoja na kugharamia huduma za mazishi kwa familia 29 zilizopoteza wapendwa wao kutokana na milipuko hiyo ya mabomu,” ameeleza.

Ametumia fursa hilo kufafanua kuwa yanapotokea majanga yanayosababishwa na nguvu za asili, ugonjwa wa mlipuko na yanayofanana na hayo, serikali hailipi fidia bali hutoa kifuta machozi kwa waathirika.